Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​DKT. SAMIA AANDIKA HISTORIA UZINDUZI WA SGR NCHINI


news title here
02
August
2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi huduma za safari za treni za abiria katika reli ya kiwango cha kimataifa - SGR, miundombinu ya reli na stasheni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, hafla ya uzinduzi imefanyika katika Stesheni ya SGR mkoani Dodoma Agosti 1, 2024.

Mhe. Rais amesema Serikali imewekeza takriban dola za kimarekani billioni 10 sawa na Shilingi trilioni 23.3 katika mradi wa SGR kwa lengo la kuboresha ustawi wa maendeleo ya wananchi kwa kasi na kupunguza gharama na muda za usafirishaji wa mizigo na abiria kutoka saa 9 hadi saa 3:30 kwa safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Mhe. Rais amesema maendeleo ni hatua kwasababu ujenzi wa reli hii ya kiwango cha kimataifa ilianza kwa maongezi kwa viongozi wa Afrika Mashariki katika Serikali ya awamu ya tatu chini ya uongozi wa hayati Benjamin Mkapa, Serikali ya awamu ya nne chini ya Mhe. Jakaya Kikwete ilifanya upembuzi yakinifu, Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa hayati John Magufuli ilianza ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa na sasa Serikali ya awamu ya sita inaendeleza mradi huu kwa falsafa ya kazi iendelee

"Reli hii ina faida nyingi italinda mazingira, itaongeza ajira, itapunguza msongamano wa magari na itaongeza ufanisi wa bandari kwasababu ya uwezo wa kubeba mzigo mwingi kwa wakati mmoja" alisema Mhe. Rais

Mhe. Rais ameipongeza Wizara ya Uchukuzi, Shirika la Reli Tanzania pamoja na wadau wote kwa usimamizi makini wa mradi huu wa kimkakati wa reli ya kiwango cha kimataifa ambao unabeba sura na ndoto kubwa ya taifa.

Mhe. Rais ametoa wito kwa Wizara ya Uchukuzi, Shirika la Reli Tanzania, wasimamizi pamoja na wakandarasi kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa

"Napenda kuwaasa wananchi wenzangu kuwa reli hii ya SGR ni tunu muhimu kwa uchumi wetu tuihifadhi, tuithamini na kuipenda" alisema Mhe. Rais

Mhe. Rais ameridhia ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Shrlirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa Stesheni ya SGR Dodoma iitwe Samia Suluhu Hassan na kutoa majina kwa stesheni za SGR Morogoro kuitwa Jakaya Kikwete, stesheni ya Dar es Salaam kuitwa John Magufuli, stasheni ya Tabora kuitwa Ally Hassan Mwinyi stesheni ya Shinyanga kuitwa Abed Karume, stesheni ya Mwanza kuitwa Julius Nyerere na stesheni ya Kigoma kuitwa Benjamin Mkapa.

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali ya awamu ya sita imekamilisha reli ya kiwango cha kimataifa kwa kilometa 722 ambazo tunazizindua leo na imeanzisha vipande vingine vya ujenzi wa hii ya SGR kwa kilometa 1560 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na reli ndefu ya SGR inayotumia nishati umeme.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amesema Shirika limenunua vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vichwa 19 vya treni ya umeme, mabehewa 89, treni za kisasa EMU seti 10 na mabehewa ya mizigo 1430 thamani ya uwekezaji huu ni wa Shilingi trilion 1.8, aidha Kadogosa ameeleza kwa kusema Shirika limeshapokea vichwa 17 vya SGR mabehewa 65 na seti 3 za treni ya kisasa EMU.

"Ulipoingia madarakani Mhe. Rais uliahidi utaendeleza ujenzi wa reli ya SGR na leo tunashuhudia ukamilishwaji na kuanza safari za abiria kati ya Dar es Salaam na Dodoma na maendeleo ya ujenzi wa vipande vingine vya reli ya kiwango cha kimataifa SGR" alisema Kadogosa

Treni ya SGR Tanzania imesanifiwa kwa viwango vya kimataifa na kuifanya Tanzania kupata tuzo mbili za kimataifa. Tangu kuanza usafirishaji wa abiria kwa treni ya kiwango cha kimataifa tarehe 14 Juni 2024 imeshasafirisha abiria laki moja na elfu themanini na nane (188,000) hii ni sawa na wastani wa abiria elfu saba (7,000) kwa siku. Safari za abiria kwa treni ya kiwango cha kimataifa zinaendelea kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Dar es Salaam hadi Dodoma m.