Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

DKT. MWINYI AFUNGUA MAONESHO YA BIASHARA ZANZIBAR, TRC YASHIRIKI


news title here
11
January
2024

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi amefungua rasmi maonesho ya 10 ya kimataifa ya Biashara Zanzibar yanayoendelea katika uwanja wa Fumba Zanzibar, Januari 10, 2024.

Shirika la Reli Tanzania – TRC ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki maonesho yenye lengo la kuwapatia wafanya biashara fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa na huduma wanazotoa pamoja na wananchi kupata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kibiashara.

Lengo la maonesho ni kutafuta wanunuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na wajasiriamali.

Dkt. Mwinyi alisema kuwa “maonesho haya ya biashara ni sehemu ya maadhimisho ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo yanatimiza miaka 60, nimefurahi kuja kuona hatua hii ya maendeleo ya ujenzi wa uwanja utakaotumika kuanzia sasa kwa ajili ya maonesho ya biashara hapa Zanzibar kila mwaka”

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amefanya mkutano na wanahabari na kuzungumzia ushiriki wa TRC katika maonesho ya Biashara Zanzibar pamoja na maendeleo ya mradi wa SGR hususani hatua zinazochukuliwa kuhakikisha maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanza huduma za SGR mwezi Julai zinafanikiwa.

Kadogosa ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa nafasi ya kushiriki maonesho, pia alieleza kwamba historia ya reli nchini Tanzania inaanzia visiwani Zanzibar ambako reli ya kwanza ilijengwa mnamo mwaka 1879 na Sultan Said Balghash kwa ajili ya shughuli za usafirishaji eneo la Bububu.

“Sisi uwepo wetu huku ni nyumbani na tunamshukuru Mhe. Rais. Dkt. Mwinyi, hivi karibuni zilizopita alizungumzia kutaka kurudisha reli Zanzibar, naamini sisi tutakuwa washiriki wakubwa katika jambo hilo na sisi tuko tayari tuna wahandisi wa kutosha, tumekuwa tukijenga reli kwa muda mrefu tunaingia mwaka wa tisa katika kujenga, tuna uzoefu wa kutosha wa kutoa ushauri katika ujenzi wa reli” alisema Kadogosa

Mkurugenzi Mkuu alipata fursa ya kutembelea mabanda ya taasisi kadhaa zinazoshiriki maonesho hayo ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini - LATRA, Mamlaka ya Bandari Tanzania, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania – TASAC na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar kujionea shughuli zinazofanywa na Taasisi hizo.

Ujenzi wa reli visiwani Zanzibar unatarajiwa kuleta manufaa makubwa ukizingatia kuwa bidhaa nyingi cha chakula ikiwemo mchele zinatoka Tanzania bara, hivyo uwepo wa reli ya kiwango cha kimataifa utasaidia pia kupunguza gharama na kuleta unafuu kwa wanunuzi wa bidhaa mbalimbali.