Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​DKT. MPANGO AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA SGR TABORA - ISAKA


news title here
19
January
2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha nne, Tabora - Isaka kilomita 165 katika viwanja vya Stesheni mtaa wa bandari, Isaka mkoani Shinyanga Januari 18, 2023.

Thamani ya mkataba wa ujenzi wa kipande hiki ni dola za kimarekani milioni 900.1 sawa na Fedha za kitanzania Trilioni 2.6, na muda wa ujenzi ni miezi 42 na mradi huu unatarajia kukamilika mwezi Machi, 2026

Makamu wa Rais ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuwapunguzia wananchi muda wa safari na gharama za bidhaa kutokana na gharama za usafirishaji wa malighafi na bidhaa pamoja ili kuboresha maisha. Dkt. Mpango amesema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa ni fursa ya kuitumia vizuri jografia ya nchi yetu ili iwe kitovu cha usafirishaji kutoka na kuingia ndani ya ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa mara mradi utakapokamilika reli itahitaji vifaa vya uendeshaji ikiwemo mabehewa ya mizigo, abiria pamoja na vichwa vya treni. Kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji, Serikali imeshaingia mikataba ya ununuzi wa mabehewa ya abiria 89, vichwa vya treni ya umeme 19, seti za treni za kisasa (Electrical Multiple Unit) 10, uwekezaji huu una thamani ya trillion 1.2 za kitanzania.

Pamoja na kupunguza gharama na muda wa usafirishaji, ujenzi wa miradi ya kimkakati imekuwa ikitoa fursa za ajira kwa wananchi, kandarasi na zabuni kwa watanzania.

“Kwa takwimu za sasa mradi umeajiri jumla ya wafanyakazi wa moja kwa moja zaidi ya 20,000 na kulipa mshahara wa dola za kimarekani milioni 102 sawa bilioni 237.9 za kitanzania, kwa vipande vitatu vinavyotekelezwa na zabuni zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 820 sawa na trilioni 1.91 za kitanzania zimetolewa na pia Serikali imekusanya kodi yenye jumla ya dola milioni 450 sawa na fedha za kitanzania shilingi trillioni 1.05” alisema Makamu wa Rais.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameeleza kuwa wawekezaji katika ujenzi wa reli ya kisasa una manufaa makubwa kwa watanzania na wanajumuiya ya Afrika Mashariki, mathalani gharama ya kontena moja kutoka nchi za Ulaya na Asia kuja bandari ya Dar es Salaam hugharimu kati ya dola za kimarekani 2,000 hadi 3,000 ikilinganishwa na kulisafirisha kwenda Congo kwa njia ya barabara hugharimu dola za kimarekani 9,000 hadi 15,000 na muda wa safari hadi siku 30 ikilinganishwa na reli hii itakapokamika kontena linaweza kuchukua safari ya hadi saa kati ya 26 na 36 kufika kindu.

Aidha, Prof. Mbarawa alibainisha mchango mkubwa uliopo katika wekezaji wa miundombinu ya reli katika kuzisaidia bandari nchini. “Reli ina mchango mkubwa kwenye miundombinu mingine ikiwemo bandari na barabara, kwani itachangia katika kuongeza ufanisi wa bandari zetu kwa kubeba mzigo mkubwa kwa wakati mmoja na kupunguza mrundikano wa mizigo bandarini pia itazipungizia uharibifu wa barabara na matengenezo ya mara kwa mara na kizifanya zidumu” alisema Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mkurugenzi Mkuu TRC, Ndugu Masanja Kadogosa alitoa taarifa ya maendeleo ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa ambapo alisema, Kipande cha kwanza Dar e salaam hadi Morogoro ujenzi umefikia asilimia 97.77, kipande cha pili Morogoro hadi Makutupora ujenzi umefikia asilimia 91.79, kipande cha tatu Makutupora hadi Tabora ujenzi umefikia asilimia 3.95, na usanifu wa kina na kipande cha tano Isaka hadi Mwanza ujenzi umefikia asilimia 22.71.

Kadogosa aliongeza kuwa, kazi iliyobaki ni kuunganisha nishati kwenye vituo vya kupozea umeme na kuuingizia kwenye mfumo wa msongo wa kilovoti 25 ambao ndio umeme unaohitajika kwenye uendeshaji, majaribio na ukakuguzi wa kazi hii unaendelea kabla ya kuingiza umeme. Kwa kipande cha Morogoro mpaka Makutupora ujenzi wa msongo wa kilovoti 220 unaendelea na una jumla ya kilomita 410 na mkataba wake ni shilingi bilioni 160.2, mpaka sasa wakandarasi amelipwa shilingi bilioni 44.5 na bilioni 29.31 kila mmoja.

“Umuhimu wa kipande hiki ni kuziunganisha nchi mbili kuitumia bandari ya Dar es salaam kwa usafirishaji na kwa umuhimu wa kipekee ni kusafirisha madini ya nikeli yaliyopo Musongati kwani bila kuwa na reli uzito wa madini haya hautaweza kusafirishwa kwa bei na gharama nafuu ikiwemo kutunza barabara zetu” alisema Kadogosa.