Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​DIASPORA KUTOKA UINGEREZA WAISIFIA SGR


news title here
29
May
2025

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema Serikali kupitia Shirika hilo imetekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kufuatia kuanza kwa operesheni kwenye mradi mkubwa wa kimkakati wa reli ya umeme (SGR) ambapo hadi sasa abiria zaidi ya milioni 2.5 wamesafiri na treni hiyo toka kuanza kwa uendeshaji wake June 14,2024.

Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameyasema hayo wakati wa safari aliyoongozana na Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye treni maalumu ya SGR wakitokea jijini Dar es Salaam kuelekea kwenye mkutano mkuu wa siku mbili wa CCM jijini Dodoma Mei 29 na 30, 2025.

Ndugu Kadogosa amesema idadi hiyo ya abiria zaidi ya Milioni 2.5 katika kipindi cha takribani miezi 9 ya operesheni ni kubwa kulinganisha na abiria 400,000 waliosafirishwa na treni ya MGR kwa kipindi cha mwaka mzima.

Aidha Ndugu Kadogosa alisema kuwa kuna umuhimu wa kutunza na kuilinda miundombinu ya reli ili kuendelea kuwa bora na imara katika kipindi chote cha matumizi vilevile amehimiza wananchi kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya usalama dhidi ya hujuma katika miundombinu ya reli.

" Reli ya mwendokasi imeundwa ili kukidhi mahitaji ya sasa na vizazi vya baadae, hivyo ni wajibu wetu kuonesha uzalendo katika kutunza na kulinda miundombinu ya reli" amezungumza Ndugu Masanja Kadogosa.

Katika hatua nyingine, akizungumza na waandishi wa habari Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa usafiri wa treni umekuwa ukisafirisha wajumbe wa CCM tangu enzi za miaka ya nyuma kuwatoa wajumbe katika mikoa tofauti na kuwafikisha Dodoma katika mkutano mkuu wa CCM,

“Hii inachagiza kukuza na kutangaza huduma zitolewazo na TRC kwani zaidi ya wajumbe 800 wa CCM wamesafiri kwa SGR kuelekea mkutano mkuu wa CCM Jijini Dodoma “ alieleza Ndugu Kadogosa.

Awali mmoja wa Watanzania 10 wanaoishi nchini Uingereza (Diaspora) waliokuja kushiriki mkutano huo Bi. Elizabeth Thomas Msabi, kwa niaba ya wenzake ameunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo ya taifa kupitia mradi huu mkubwa wa kimataifa wa SGR.

" Usafiri umekuwa rahisi sana kwa maana ni mara ya kwanza kusafiri na treni ya mwendokasi, haya ni miongoni mwa maendeleo makubwa natoa pongezi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pia natoa wito kwa watanzania waliopo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali " alisema Bi. Elizabeth Thomas Msabi.

TRC inaendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa SGR kwa vipande vilivyobaki ili kuiunganisha Mikoa ya Tanzania pamoja na nchi za jirani ambapo hadi sasa utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kipande cha saba na kipande cha nane kutoka Uvinza hadi Msongati hivyo kuendelea kurahisisha huduma za usafirishaji kwa kutumia treni ya SGR.