DC UYUI AWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KATIKA ZOEZI LA UTWAAJI ARDHI
April
2023
Mkuu wa Wilaya ya Uyui Ndugu Zakaria Mwansasu amewataka wananchi wa kijiji cha Malongwe kutoa ushirikiano kwa timu kutoka Shirika la Reli Tanzania - TRC katika zoezi la utwaaji ardhi linaloendelea mkoani Tabora, Aprili 2023.
Ndugu Mwansasu alizungumza na wananchi katika mkutano wa uhamasishaji uliofanyika kwaajili ya maandalizi ya utwaaji ardhi kupitia uhamishaji wa makaburi yaliyopitiwa na mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha tatu Makutupora – Tabora kwa lengo la kumpatia eneo mkandarasi aweze kuendelea na ujenzi.
“Serikali inajenga miundombinu, ni ya kwetu na inatumia fedha nyingi, hivyo nawaomba mtoe ushirikiano kwa timu hii na asiwepo mtu yeyote atakayekwamisha zoezi” alisema Mwansasu
Mhandisi Rajab Mahaja kutoka TRC alifafanua utaratibu wa uhamishaji makaburi ambapo makaburi yaliyopitiwa na mradi yataainishwa na kuhamishwa kwa kuzingatia taratibu za afya kupitia wataalamu wa afya wa Wilaya na kuhamishiwa katika maeneo rasmi kwa kufuata taratibu za imani ya Dini husika.
“Maeneo yatakayochukuliwa kwaajili ya ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa yatahusisha maeneo kwaajili ya kuchukua kifusi, maeneo ya kutupa kifusi kisichofaa kwa ujenzi na maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya reli” aliongeza Mhandisi Mahaja.
Mtaalamu wa Afya kutoka Wilaya ya Uyui Bi. Mary Kayombo aliwasisitiza wananchi kujitokeza siku ya zoezi la uhamishaji ili kuhakikisha makaburi yanahamishiwa katika maeneo rasmi yaliyopangwa na Serikali ya kijiji. Vilevile aliwasihi wananchi kuacha kuzika katika maeneo ya makazi ili kuepusha uhamishaji wa makaburi katika maeneo ya makazi pindi miradi ya maendeleo inapotaka kutekelezwa.
Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa Dar es Salaam kuelekea Mwanza na Kigoma. Miongoni mwa shughuli za awali za utekelezaji wa mradi ni utwaaji wa ardhi ili kukabidhi maeneo kwa mkandarasi aweze kuendelea na ujenzi. Mradi wa SGR unatekelezwa kwa mtindo wa sanifu jenga, hivyo zoezi la utwaaji ardhi ni endelevu kulingana na mahitaji ya mkandarasi.