Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​DC CHAMWINO ASISITIZA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA SGR


news title here
12
April
2024

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Bi. Janeth Mayanja kwa kushirikiana na maafisa wa TRC wameongoza zoezi la kampeni ya uelimishaji jamii kuhusu uwashaji wa umeme katika kipande cha pili Morogoro - Makutupora katika reli ya kiwango cha kimataifa kwa wananchi katika mkutano uliofanyika kata ya Igandu mkoani Dodoma tarehe 9 Aprili 2024.

Bi. Janeth Mayanja amesema maafisa wa TRC wametoa elimu kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi ambapo wananchi wamesisitizwa kutumia vivuko maalumu vilivyowekwa na mkandarasi ambavyo ni vivuko vya juu na chini pamoja na vivuko maalumu vya kuvushia wanyama kwaajili ya usalama wao.

"Ningependa kusisitiza hivi vipeperushi na alama za usalama wa reli mlizoonesha hapa kwenye mkutano mkavibandike mashuleni, ofisi za serikali za vijijiji na mitaa na maeneo yenye mikusanyiko ili kuwawezesha wananchi kujifunza zaidi" ameongeza Bi. Janeth.

Mhandisi wa Mradi wa kipande cha pili Morogoro - Makutupora Bi. Christina Samueli amesema kampeni hii ni maalumu kwaajili ya kuelimisha na kujulisha Jamii TRC imekaribia kuwasha umeme kwenye njia ya reli na kuanza majaribio ya uendeshaji wa treni kutoka Morogoro hadi Dodoma.

"Mkandarasi akijihakikisha miundombinu yote ya umeme ipo sahihi tutaanza majaribio ya kupitisha treni ili kuendana na agizo la Mheshimiwa Rais wetu kuhakikisha hadi Julai reli ianze kufanya kazi" amesisitiza Mhandisi Christina.

Mhandisi Chacha Marwa kutoka Wizara ya Uchukuzi amewasisitiza wananchi wa Igandu kutunza mazingira na miundombinu ya reli katika mradi huu wa kimkakati ili kufikia lengo la uendeshaji wa treni ya SGR, pia amewapongeza TRC kwa kuandaa zoezi la uelimishaji jamii kabla ya kuanza uendeshaji wa treni ya mwendokasi.

"Napenda kuwasihi wananchi na watoto wasikate fensi zilizowekwa kwaajili ya ulinzi wa reli yetu na wao wenyewe kwani usalama unaanza na wewe chukua tahadhari" amesema Mhandisi Chacha.

Timu ya wataalam kutoka TRC hadi Sasa imefanya kampeni kwa awamu ya kwanza katika Kata za Dodoma Jiji ambazo ni Tambukareli, Ntyuka, Kilimani, Miganga, Iyumbu, Kikombo na Ihumwa awamu ya pili zoezi limefanyika Wilaya ya Mpwapwa katika Kata za Kimagai, Kisisi, Godegode, Msagali, Gulwe na Pandambili, awamu ya tatu Wilaya ya Kilosa katika kata 13 ambazo ni Munisagara, Mzaganza , Mwasa, Kikundi, Kidete, Magomeni, Mbumi, Kasiki, Mkwatani, Chanzuru, Mabwerebwere, Kimamba, Mkata na wilaya ya Mvomero katika kijiji cha Kimambila na zoezi hili litaendelea katika Wilaya ya Bahi na Manyoni.

Naye Afisa Jamii kutoka TRC Bi. Lightenes Mngulu amesema katika maeneo ambayo vivuko havijakamilika kipindi cha majaribio kutakua na vivuko vya muda vilivyoanishwa na mkandarasi ambavyo vitakua vinapita juu ya reli na kutakua na watu wa vibendera kwaajili ya kuruhusu na kuzuia wananchi kupita juu ya reli kwaajili ya usalama wao.

"Uendeshaji utakapoanza vile vivuko vya muda vyote vitatolewa na kufungwa kwa sababu vivuko maalumu vilivyoanishwa na Mkandarasi vitakua tayari vimekamilika na wananchi watatakiwa kutumia vivuko vya juu ama vya chini na wakumbuke Usalama unaanza na wewe chukua tahadhari" amesisitiza Bi. Lightness.

Ujenzi wa kipande cha pili Morogoro - Makutupora Hadi sasa kimefikia asilimia 96.61 na mkandarasi anaendelea na ujenzi wa hatua za mwisho.