CHUO CHA TEKNOLOJIA YA RELI NCHINI CHAFANYA MAHAFALI YA KWANZA

December
2021
Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania – TIRTEC chafanya mahafali ya kwanza kwa wahitimu wa ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa wahitimu wa taaluma mbalimbali, mahafali hayo yamefanyika katika viwanja vya chuo cha reli mkoani Tabora, Disemba 18, 2021.
Chuo cha Teknolojia ya Reli kilianzishwa mwaka 1947 na wakoloni na baadaye kuendelea kusimamiwa na Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa lengo la kuwapa mafunzo watumishi wa Shirika la Reli na kuandaa wataalamu wa kada mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa huduma za Shirika la Reli.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahaya Nawanda ambaye alikuwa mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TRC Bi. Amina Lumuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Washauri ya Chuo Mhandisi Alfred Ng’hwani, wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo, Mkuu wa Chuo Bwana Damas Mwajanga, wafanyakazi wa chuo, wahitimu na wanafunzi.
Chuo cha Reli Tabora kinatoa kozi mbalimbali katika ngazi ya Astashahada na Stashahadakatika kada ya usafirishaji, teknolojia ya matengenezo ya njia ya reli, ukaguzi na matengenezo ya behewa pamoja na kozi za muda mfupi kwa ajili ya watumishi wa Shirika la Reli pamoja na watumishi wa taasisi nyingine zinazohusika na usafiri wa reli ikiwemo Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia – TAZARA na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchikavu – LATRA.
Akihutubia katika Mahafali hayo Mkuu wa Chuo Bwana Damas Mwajanga ameeleza kuwa Shirika la Reli kupitia Chuo cha Reli lina mpango wa kuboresha miundombinu ya chuo hicho ili kiweze kuzalisha wataalamu wengi zaidi na kuanzisha kozi mpya ili kukidhi mahitaji ya sasa hususani katika shughuli za uendeshaji wa reli ya kisasa – SGR pamoja na kuwawezesha wahitimu kujiajiri.
Bwana Mwajanga ameongeza kuwa pamoja na changamoto kadhaa, Chuo cha Reli kimeweza kufanikiwa kuunda bodi ya ushauri ya chuo, kuboresha taaluma, kujenga uzio, kuimarisha nidhamu ya wanafunzi, kushiriki katika makongamano ya kitaaluma, kusajili chuo na kupewa ithibati pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi.
Bi. Amina Lumuli, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TRC amesema kuwa Shirika limepokea changamoto na linaahidi kuendelea kuzitatua changamoto ili kuboresha mazingira ya chuo ambapo, Bi. Amina aliongeza kuwa Shirika tayari limeanza kushughulikia baadhi ya changamoto ikiwemo changamoto ya usafiri pamoja na ujenzi wa miundombinu ya chuo ambazo kupitia mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa Makutupora - Tabora changamoto hizo zitashughulikiwa.
Naye Mgeni Rasmi katika Mahafali hayo Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahaya Nawanda ameahidi kuendelea kushirikiana na Chuo cha Reli ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa chuo muda wote, na kulitaka Shirika la Reli kushughulikia changamoto zilizopo ili kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.