Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BODI YA WAKURUGENZI WA SHIRIKA LA RELI YA UGANDA YATEMBELEA TRC


news title here
26
January
2023

Shirika la Reli Tanzania limetembelewa na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Uganda (URC) jijini Dar es Salaam katika Stesheni ya SGR kwaajili ya kuona maendeleo ya miundombinu ya SGR, Januari 2023.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro amesema nchi ya Tanzania na Uganda zimekua zikishirikiana kibiashara kwa muda mrefu vilevile TRC husafirisha mizigo kupitia reli ya kati hadi Mwanza kwaajili ya kupeleka Uganda na Sudani ya Kusini.

"Katika kuongeza ushirikiano TRC imewahi kujenga kipande cha reli nchini Uganda chenye urefu wa kilomita 14 kwahiyo ujio huu wa leo ni kuendeleza ushirikiano uliopo toka zamani na leo wamekuja kujionea maendeleo ya mradi wa reli ya kisasa na wamejifunza mambo mengi kuhusu ujenzi wa SGR" alisema Kondoro.

Kaimu Mkurugenzi wa TRC Bw. Vincent Tangoh ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya URC kwa kuitembelea TRC na kaipongeza Uganda kwa kuweka lengo la kuanza ujenzi wa SGR nchini humo na ameahidi TRC itawapa ushirikiano kupitia uzoefu iliyopata kwenye ujenzi wa reli ya kisasa.

"Wamejionea maendeleo ya mradi kwa kipande cha kwanza ambacho ni Dar es Salaam - Morogoro na kimewapa hamasa kubwa kwa namna kilivyojengwa pamoja na stesheni zake, pia wameona kipande cha pili kimebaki asilimia chache kukamilika ambacho ni Morogoro - Makutupora" alisema Tangoh.

Mwenyekiti wa bodi ya URC Ndugu Alhaji Abdullatif Wangubo amesema bodi imetembelea TRC kwaajili ya kuona maendeleo ya mradi wa SGR pamoja na kujifunza usimamiaji wa usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya reli kupitia reli ya kati na vilevile matarajio ya namna SGR itakavyokua inasafirisha abiria na mizigo ya kibiashara.

"Naipongeza TRC na Serikali ya Tanzania kwa kuweza kusimamia ujenzi wa mradi huu wa reli ya kisasa kwa uaminifu mkubwa na kuweza kufikia hatua hii kubwa, hata sisi tumejifunza hapa kuhusu ujenzi wa SGR" aliongeza Alhaji Wangubo.

Mkurugenzi Mkuu wa URC Stephen Wakasenza ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na TRC kwa kazi kubwa waliyofanya kusimamia ujenzi wa SGR, Pia amesema Uganda kwasasa inatumia reli ya MGR pekee katika usafirishaji lakini Serikali imesaini Mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kisasa na kampuni ya Yapi Merkezi.

"Tunategemea kuanza ujenzi kwa kuanzia na eneo la Malaba - Kampala vilevile Serikali imepanga kujenga SGR kati ya Kampala na Kasese ili kuunganisha eneo la magharibi mwa nchi ya Uganda" aliongeza Wakasenza.