BODI YA WAKURUGENZI TRC YAMALIZA ZIARA KUKAGUA MRADI WA SGR
September
2023
Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Reli Tanzania – TRC yamaliza ziara kukagua mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza iliyofanyika kuanzia Septemba 15 hadi 19, 2023.
Bodi ya wakurugenzi TRC imefanya ziara kukagua mradi kwa lengo la kuona maendeleo ya mradi, kujifunza pamoja na kutambua changamoto za mradi kwaajili ya kutoa muongozo na maelekezo ya kuhakikisha changamoto zinatatuliwa na mradi unakamilika kwa wakati.
“Tuko kwenye ziara na bodi mpya ya wakurugenzi, tumeanzia kipande cha kwanza na leo tunamalizia kipande cha tano lengo ni kupata uelewa wa kinachoendelea ili waweze kujua wapi wataanzia pale ilipoishia bodi iliyomaliza muda wake” alieleza Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bi. Amina Lumuli
Mwenyekiti na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi TRC waliambatana na menejimenti ya Shirika la Reli pamoja na wahandisi mbalimbali kwaajili ya kupata taarifa za maendeleo ya mradi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya reli, mifumo ya mawasiliano, ishara na umeme pamoja na maandalizi ya vifaa kwaajili ya shughuli za uendeshaji ambavyo ni mabehewa na vichwa vya treni.
Mwenyekiti wa Bodi Bwana Ally Karavina amesema kazi za mradi zinaendelea vizuri ziko ndani ya muda na amewaahidi watanzania mradi kukamilika kwa wakati. Mwenyekiti alieleza kuwa Miradi ya kimkakati ni miradi itakayobadilisha uchumi wa nchi kwenda kwenye uchumi wa juu ikiwemo mradi wa SGR.
Mradi wa SGR awamu ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza wenye vipande vitano unaendelea sambamba na uagizwaji wa mabehewa na vichwa kwaajili ya kuanza shughuli za uendeshaji pindi mradi utakapokamilika.
“Utengenezaji wa mabehewa unaendelea vizuri, tumeshapokea mabehewa 14 mapya lakini leo tuna mabehewa mengine mapya 15 yameanza kushushwa, pia tumepokea mabehewa 6 ya ghorofa. Kwahiyo kwa upande wa mabehewa hakuna shida, kichwa cha kwanza cha treni tunatarajia kukipokea mwanzoni mwa mwezi Novemba ili tuanze majaribio” alisema Bi. Amina
Bi. Amina alisisitiza kuwa watanzania wategemeea huduma nzuri, Shirika limejipanga kwa wataalamu wanaopata mafunzo ndani na nje ya nchi pia maandalizi yanaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri zenye ubora unaostahili.
Sambamba na ziara Bodi imeanza mafunzo ya siku mbili jijini Mwanza kwaajili ya kuwajengea uwezo kuhusu namna ya kusimamia Shirika, Sheria pamoja na taratibu za kiutendaji katika shughuli za Bodi na Shirika kwa ujumla.