Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BODI YA WAKURUGENZI TRC YAKAGUA RELI YA ZAMANI DAR – KALIUA


news title here
14
December
2023

Bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania TRC imekagua njia ya reli ya MGR Dar es Salaam hadi Kaliua, Disemba 2023.

Mwenyekiti wa bodi ya TRC Bw. Ally Karavina ameeleza kuwa licha ya changamoto mbalimbali za hali ya miundombinu, njia hiyo ya reli ni muhimu katika kuunganisha bandari ya Dar es Salaam nan chi Jirani kupitia usafirishaji wa mizigo.

“ Tunataka kuwa na usalama zaidi wa vyombo vinavyopita katika njia hii, ziara hii itatusaidia kupata hali halisi ya njia na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo ili njia hii ya reli itusaidie kuongeza mapato ya Shirika” aliongeza Bw. Karavina.

Aidha Bw. Karavina ameeleza kuwa mipango iliyopo ni kufanya ukarabati wa njia hiyo ya Reli ikiwa ni Pamoja na uboreshaji wa tuta la reli, uwekaji wa mataruma ya zege na ukarabati wa makaravati na madaraja.

Kwa upande wake mjumbe wa bodi Dkt. Shaban Mwinjaka, ameeleza kuwa Pamoja na ujenzi wa reli ya kiwango cha SGR, bado reli ya zamani (MGR) inahitajika na ina mchango mkubwa katika usafirishaji wa abiria na mizigo.

“Reli hizi mbili zitakuwa zinasaidiana katika usafirishaji wa abiria na mizigo, hatuwezi kuacha kuitumia reli hii na Tanzania sio nchi pekee ambayo reli ya kiwango kama hiki bado inaendelea kutumika” alisema Dkt. Mwinjaka.

Pamoja na wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi, menejimenti ya TRC imeshiriki ukaguzi huo wa miundombinu, ambapo Mkurugenzi wa Miundombinu, Mhandisi Machibya Masanja ameeleza jitihada ambazo zinafanywa na shirika ili huduma ya usafiri wa reli iendelee licha ya mvua zinazoendelea kunyesha.

“tuna kipande cha Kilosa – Gulwe ambacho kimekuwa kikiathiriwa na mvua mara kwa mara, hadi sasa hatua tulizochukuwa ni kutafuta suluhisho la kudumu ambapo tumeanza na ujenzi wa daraja la mita 175 kati ya Godegode na Gulwe, lakini pia tunaanza ujenzi wa mabwawa yatakayosaidia kudhibiti maji yam to Mkondoa” alisema Mhandisi Machibya.

Kupitia ziara hiyo inayolenga kukagua hali ya miundombinu ya Reli ya zamani (MGR) wakati ambapo mvua zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, wajumbe wa bodi wanatarajiwa pia kufika Mpanda mkoani Katavi na Kigoma wakitumia usafiri wa Kiberenge.