BODI YA WAKURUGENZI NEMC YARIDHISHWA NA HATUA ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA KATIK MRADI WA SGR

April
2019
Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Usimamizi wa Mazingira – NEMC yafanya ziara katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa Dar es Salaam – Singida Makutupora. Lengo la kukagua mazingira pamoja na hatua zinazochukuliwa na Mkandarasi kuhifadhi mazingira katika maeneo ya mradi, hivi karibuni Aprili 2019.
Katika ziara hiyo Wajumbe wa Bodi ya NEMC wakiongozwa na Mwenyekiti Prof. Esnath Osinde Chagu walipata fursa ya kuona hatua mbali mbali za uhifadhi mazingira zinazochukuliwa na Mkandarasi Yapi
Merkezi wakati wa ujenzi wa reli, madaraja,stesheni, mahandaki na makalavati bila kuathiri mazingira ya wakazi wanaozunguka maeneo ya mradi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NEMC Mhandisi Prof. Esnat Osinde Chaggu amesema kuwa ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Mkandarasi kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa wakati wa ujenzi na pindi utakapokwisha kwani ameshuhudia vibao vinavyoelekeza umuhimu na jinsi ya kutunza mazingira katika mradi.
Amesema Mhandisi Prof. Esnat Osinde “Tumeridhishwa sana na tunaona kwamba kampuni ambayo imepata hii kazi inafanya juhudi kubwa sana ya kuhakikisha mazingira yanakuwa vizuri, kila mahali tulipokuwa tukipita tumeona vibao mbali mbali vinavyoelekeza umuhimu wa kuangalia mazingira na usalama kwanza”
Akizungumza na TRC Reli TV Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira – NEMC Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka Mafwenga amesema kuwa amefurahishwa na mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kwa kuwa hakujawahi kutokea mradi mkubwa kama wa SGR na ameipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu wa utekelezaji wa mradi wa SGR.
Amesema Dkt. Samuel Gwamaka “Nimefurahishwa na mradi huu mkubwa ambao hatujawahi kuwa nao toka enzi ya uhuru, ni mradi ambao unazidi sekta nyingine zote, ninaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa hatu hii ya mradi, watanzania tunajivunia kwa hilo”
Baraza la Usimamizi wa Mazingira – NEMC lina jukumu la kufahamu changamoto za mazingira na namna Miradi inavyoweza kutekelezwa bila kuathiri Mazingira pamoja na kutoa idhini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi baada ya kujiridhisha na tathmini ya mpango kazi wa uhifadhi wa mazingira wakati wa mradi.