Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BODI YA WAKURUGENZI LATRA YAPONGEZA MAANDALIZI YA SGR


news title here
02
February
2024

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini - LATRA imetembelea Shirika la Reli Tanzania - TRC katika ofisi za makao makuu TRC na stesheni ya reli ya kiwango cha kimataifa - SGR Pugu jijini Dar es salaam tarehe 01 Februari 2024.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Bwana Ally Karavina amesema LATRA na TRC wamekutana kwaajili ya kuzungumza kuhusu maandalizi ya kuanza uendeshaji wa SGR.

"Hali ya maandalizi kwa sasa ni nzuri kuanzia kiufundi, Sheria, utayarishaji wa nauli pamoja na watoa huduma wetu nao wapo vizuri na wanaendelea na mafunzo namna ya kuhudumia abiria katika kiwango kizuri cha kimataifa" alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Bwana Ally Karavina.

Lengo la ziara ni kuona maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa unaosimamiwa na Shirika la Reli Tanzania ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza hadi sasa Dar es Salaam - Morogoro 98.78%, Morogoro - Makutupora 96.15%, Makutupora - Tabora 13.23% Tabora - Isaka 5.33% na Isaka - Mwanza 50.51%.

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi LATRA Profesa Ahmed Ame amesema LATRA ina majukumu makubwa katika usafiri wa reli ikiwemo udhibiti wa mtoa huduma (TRC), utoaji huduma wa Shirika na miundombinu ya reli.

Pia Mwenyekiti Profesa Ahmed Mohamed Ame amesisitiza utayari wa kitaalamu katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa pindi ifikapo julai 2024 treni za abiria za SGR Dar es Salaam hadi Dodoma ziwe zimeanza kutoa huduma ya usafiri.

Kaimu Mkurugenzi wa TRC Ndugu Senzige Kisenge amesema "LATRA ni mdhibiti wa huduma za TRC na tumezungumza kuhusu kukamilisha masuala ya nauli na leseni na tumejadiliana vizuri na tutakamalisha kwa wakati pia Bodi ya wakurugenzi wameweza kuona maendeleo na utayari wa miundombinu ya SGR".

"Maandalizi yanaendelea vizuri na kwa kiasi kikubwa tunakamalisha majaribio ya njia, mabehewa pamoja na vichwa vya treni yanaendelea kufanyika" amesisitiza Senzige Kisenge.

Naye Mkurugenzi wa LATRA CPA Habibu Suluo amesema LATRA ilikua inasubiri kuona mabehewa ambapo wameona kuna mabehewa ya daraja la uchumi na daraja la biashara hivyo LATRA inaenda kukamilisha upangaji wa nauli kupitia madaraja hayo.

"Tumeridhika na maandalizi yaliyofanywa na TRC kwahiyo tunaenda kukamilisha suala la nauli pia tunaomba wananchi wayaone haya mabehewa ili siku tukitangaza nauli za SGR iwe Kila mtu anaelewa daraja la kiuchumi lipoje na la biashara lipoje"

Pia Mkurugenzi CPA Habibu Suluo ameipongeza TRC kwa kuweza kusimamia mradi huu mkubwa na vile vile ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha ujenzi unakamilika.

Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha TRC inaanza uendeshaji mapema kabla ya mwezi Julai 2024. Hali hiyo imethibitishwa na namna LATRA na TRC zilivyojipanga kushirikiana kuelekea utoaji huduma bora za usafiri wa reli.

TRC imepewa dhamana na Serikali kusimamia mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa ambapo imeanza na ujenzi wa awamu ya kwanza Dar es Salaam hadi hadi Mwanza na kipande cha kwanza cha awamu ya pili Tabora - Kigoma mradi unaotarajiwa kubadilisha uchumi wa mtanzania na Taifa kwa ujumla pindi utakapoanza uendeshaji.