BODI YA WAKURUGENZI KUTOKA LATRA WATEMBELEA MRADI WA SGR

April
2023
Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni wa bodi ya wakurugenzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini - LATRA ambao wametembelea ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro kwenye jengo la stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam Aprili, 2023.
Mwenyekiti wa Bodi kutoka LATRA Prof. Ahmed Mohamed ameeleza kuwa Shirika la Reli limejipanga vizuri hasa katika masuala ya kiusalama kutokana na mifumo ya mawasiliano ambapo walitembelea katika chumba cha ishara na mawasiliano ndani ya jengo la stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam.
“Suala la uendeshaji wa reli linategemea sana usalama wa njia na vivuko pamoja na mapishano ya njia ya reli na barabara na kubwa zaidi kuweka uzio katika njia ya reli” alisema Prof. Ahmed.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Bw. Senzige Kisenge alisema kuwa ugeni huo una manufaa makubwa katika uendeshaji wa mradi wa SGR kwa kupokea ushauri na maboresho ambayo yatauwezesha mradi kuwa bora.
Aidha Bw. Senzige alieleza kuwa TRC inaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu ambapo hadi sasa wataalamu 14 wapo nchini Korea Kusini na pia kuna mafunzo yanayotolewa ndani na mkandarasi ambapo wanafundishwa jinsi ya kuendesha mifumo mbalimbali.
“Mafunzo ni mengi ikiwemo ya umeme, mawasiliano na bado tutaendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu kwa awamu ili uendeshaji unapoanza tayari tuwe na wataalamu wa kutosha” alisema Bw. Senzige.
TRC inaendelea kusimamia mradi huo wa SGR kwa kuzingatia usalama wa watu pamoja na wanyama na kuendeleza mipango mbalimbali ya kutoa uelewa kwa wananchi kabla na baada ya mradi kuanza uendeshaji.