Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BODI YA SHIVYAWATA YARIDHISHWA SGR ILIVYOZINGATIA MAHITAJI YA WATU WENYE ULEMAVU


news title here
31
October
2021

Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) imetembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro ambapo mradi umefikia 94%, Oktoba 30, 2021.

Ziara imeanzia Km 0 katika stesheni ya SGR Dar es Salaam na kufikia tamati katika stesheni ya SGR Morogoro. Lengo la ziara ikiwa ni kukagua miundombinu ya reli ya kisasa - SGR ilivyozingatia mahitaji na huduma za watu wenye ulemavu, na mara baada ya kukagua ni kufanya tathimini ya kile ambacho wameona na kutoa maoni ili Shirika liweze kuboresha miundombinu hiyo na kuwa rafiki.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania Bw Ernest Kimaya kwa niaba ya wajumbe wa chama hicho mara baada ya ziara kumalizika amesema kuwa wameridhishwa na miundombinu ya SGR ilivyozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, hivyo kuyataka makampuni na mashirika ya umma hasa yale ya usafirishaji ndani na nje ya nchi kuja kujifunza kupitia mradi huu wa SGR.

“Tumeanza ziara yetu kuanzia stesheni ya SGR Dar es Salaam mpaka hapa Morogoro, tumeona maendeleo ya mradi na tumesikia uko mbioni kukamilika, tulipongeze shirika letu la reli hasa kwa ujenzi wa stesheni ambao umezingatia makundi ya watu wote hata sisi ambao tuna ulemavu, tumeona changamoto chache sana hasa kwa watu wasiosikia na kuona tuna imani maoni yetu yatafanyiwa kazi maana Serikali yetu ni sikivu” alisema mwenyekiti wa SHIVYAWATA.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania Bw. Ernerst aliongeza kuwa “Nchi nyingi za Afrika na hata taasisi za Serikali na binafsi zina jambo la kujifunza kupitia hiki kilichofanywa na TRC hasa katika ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika kujenga miundominu ambayo ni rafiki kwa makundi yote ya wantanzania.

Kwa upande wake Bw. Musa Kabimba, Katibu Mkuu wa Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) katika kutoa ushauri kwa Shirika la Reli aligusia suala la kuwepo mkalimani wa watu wasiosikia katika stesheni na katika upande wa mabehewa wakati wa safari ili kuhakikisha watu hao wanapata taarifa sahihi wawapo safarini.

“Yapo mambo mengi tumeona hasa tumeangalia mahitaji pamoja na huduma za watu walemavu kwa kiwango kikubwa mambo yote yamezigatiwa vipo vitu vichache sana vya kutoa ushauri hasa katika namna ya utoaji taarifa, kwa mfano kunatakiwa kuwe na mkalimani katika picha zinazotembea (video) ili kuwasaidia wenzetu wenye ulemavu wa kusikia” alisema Bw. Musa Kabimba.

Naye Bi. Nuru Awadhi ambaye Mwenyekiti wa wanawake na watoto Shirikisho la Vyama watu wenye Ulemavu Tanzania amekuwa na haya ya kuzungumza.

“Nipende kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirika la Reli Tanzania, tumepita kwenye vituo vikubwa na vidogo, wamekidhi mahita ya walemavu kwa asiliama 90. Lakini maoni yangu SGR ikianza kufanyakazi wazinagatie fulsa za ajira na biashara kwa kuwapa kipaumbele walemavu kwani nao wana wajibu wa kuchangia pato la taifa” alisema Bi. Nuru.

Hata hivyo, Bw. Abudulaziz Shambe, Katibu Mkuu wa Chama cha Watu wenye ulemavu wa Uti wa Mgongo Tanzania mara baada ya ziara kukamilika alikuwa na haya ya kuzungumza.

“Tumpongeze Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kweli mradi huu ni wa kipekee sana. Nafikiri nchi za wenzetu watakuja kujifunza Tanzania, tumeona nchi za wenzetu wamejenga SGR lakini kuna maboresho makubwa tofauti na huu wa kwetu, kwanza mradi huu ni shirikishi hasa kwa watu wenye ulemavu kwanzia vituo vyake, njia zake, tulitegemea baada ya kukagua mradi huu tutalikosoa shirika lakini kwa kweli hatuna kasoro tuliyoiona isipokuwa kuwapongeza” alisema Bw. Abudulaziz.