Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BODI YA BOT YATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA RELI YA SGR


news title here
25
April
2023

Bodi ya Wakurugenzi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wakiongozwa na Gavana wa Benki hiyo Bwana Emmanuel Tutuba watembelea ujenzi wa reli ya kiwango.cha kimataifa - SGR kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam - Morogoro katika Stesheni ya Dar ss Salaam, Aprili 2023.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua na kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali katika jitihada za kuendeleza na kukuza sekta ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia ukuaji wa uchumi miongoni mwa sekta hizo ni Reli na Bandari.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Ndugu Emmanuel Tutuba amesema kuwa BOT itahakikisha inabuni mbinu na kuunda mikakati ambayo itawezesha nchi kupata fedha za kigeni kupitia sekta za kiuchimu ambazo Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuzijenga na kuziendeleza ikiwemo mradi wa ujenzi wa SGR.

"Kwa mujibu wa Sheria BOT tunawajibu na dhamana ya kusimamia masuala mbalimbali ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuangalia mapato hasa namna tukavyoweza kupata dola za kimarekani au fedha za kigeni, tumeona namna ambavyo serikali imewekeza kwenye SGR, eneo la Kwala kuna maeneo ambayo reli hii itafika kwenye viwanda na bandari kavu eneo la TPA ambalo litaunganishwa na reli na kuchukua mzigo kwenda maeneo mbalimbali na nchi za nje, hii italeta fedha nyingi za kigeni na kusaidia nchi kukua kiuchumi" Amesema Bwana Tutuba.

Aidha, Bwana Tutuba ameongeza kuwa BOT imeshauriana na TRC, TPA pamoja na EPZA kuunda mipango na mikakati itakayowezesha uchumi wa wananchi, mashirika, makampuni pamoja na mapato ya Serikali na nchi kwa ujumla kuunganishwa kwa pamoja ili kuboresha biashara ya Kimataifa kwa kukuza mauzo ya nje na kupata fedha za kigeni.

"Uwekezaji huu wa SGR ni kweli umelenga kukuza uchumi, tulikuwa tunashauriana namna ambavyo uchumi wa mtu mmoja moja, uchumi wa makampuni, uchumi upande wa Serikali yaani mapato na nchi kwa ujumla utakavyoweza kuunganishwa ili tukuze mauzo ya kwenda nje, tukiongeza mauzo nje tunapata fedha nyingi za kigeni, kwa hiyo kuna mpango ambao tunaendelea kuangalia kama Benki Kuu kwa kushirikiana na serikali unaitwa mkakati wa Kukuza mauzo nje (import substitution initiative) na kuangalia mbadala wa vile vitu tunavyoingiza ndani kutoka nje viweze kuzalishwa ndani" Amesema Bwana Tutuba.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Bwana Mrisho Mrisho amesema kuwa ufanisi wa Bandari unategemea zaidi miundombinu thabiti hasa reli ambayo inaweza kuiunganisha bandari na maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa kuleta mizigo bandari na pia kuitoa mizigo bandarini.

"Tunatakiwa kufahamu kuwa ufanisi wa bandari unategemea zaidi miundombinu inayounganisha bandari, hata kabla ya SGR tulikuwa tuna reli ya TAZARA na ile ya zamani ya TRC kwahiyo kwa reli hii ya SGR ambayo ina ubora wa kimataifa maana yake ubebeji wa mizigo bandarini utaongezeka mara dufu kuliko hivi sasa" Amesema bwana Mrisho.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Bwana Senzige Kisenge ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania kwa kutembelea ujenzi wa SGR na kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kuishauri TRC mambo mbalimbali yatakayosaidia kuleta na kuongeza mapato pindi shughuli za uendeshaji zitakapoanza hivi karibuni.