Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BODI MPYA YA WAKURUGENZI TRC YAANZA KAZI RASMI


news title here
16
September
2023

Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania - TRC imeanza kazi rasmi kwa kukagua mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, Septemba 15, 2023.

Bodi ya Wakurugenzi ikiongozwa na Mwenyekiti Bwana Ally Karavina pamoja na wajumbe ambao ni Bwana Plasduce Mkeli Mbossa, Dkt. Shaaban R. Mwinjaka, Bwana Shaaban Ahmed Kabunga, Bwana Redemptus Peter Rugomola na Bwana Narcis Aloyce Lumumba wameanza ziara ya ukaguzi wa mradi wa SGR kwa lengo la kuona namna mradi wa SGR unavyosimamiwa na hatua iliyofikiwa.

Mwenyekiti wa Bodi Bwana Karavina amesema kuwa "SGR ni mradi wa kimkakati, sisi kama bodi ni muhimu tufanye haraka kujiridhisha na kuona maendeleo ya mradi, kupata uelewa na kuwasikia wajenzi wanasemaje ili tutakapokuja kukaa tujue wanahitaji nini ili tuweze kutoa maamuzi"

Bodi ilipata fursa ya kukagua kipande cha reli inayoingia bandarini ikianzia Ilala ambayo ujenzi wake unaendelea, pia Bodi ilikagua jengo la stesheni ya Dar es Salaam, Pugu, Morogoro, Karakana eneo la Kwala pamoja na mabehewa mapya 14 ya abiria na mabehewa mengine sita ya ghorofa kwaajili ya abiria.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi wameipongeza TRC kwa kazi kubwa iliyofanywa kusimamia vema miradi wa SGR na kuitaka iendelee kusimamia vema mradi ili kuboresha huduma za usafiri wa reli nchini

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bi. Amina Lumuli amesema kuwa dhumuni kubwa la ziara ni kujiridhisha na kazi iliyofanywa na bodi iliyomaliza muda wake pamoja na menejimenti na makandarasi ili kutimiza ndoto ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya reli nchini.

"Huu uwekezaji uliofanywa ni wa watanzania, tumejifunza mengi kutoka.kwa bodi tuna wataalamu wa nyanja mbalimbali hivyo sisi kama menejimenti tutakwenda kushirikiana na bodi ili kutatua changamoto ili kutimiza malengo ya Serikali" aliongeza Bi. Amina

Bodi mpya ya wakurugenzi TRC inatarajiwa kuendelea na ziara ya ukaguzi katika vipande vya mradi wa SGR Morogoro - Makutupora, Makutupora - Tabora, Tabora - Isaka na Isaka - Mwanza ili kupata uelewa na kuona maendeleo ya mradi na baadaye kufanya kikao maalumu cha mafunzo elekezi kabla ya kuendelea na majukumu ya kuongoza Shirika.