Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BENKI YA TCB YARIDHISHWA MAENDELEO YA MRADI WA SGR


news title here
24
August
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni wa menejimenti kutoka benki ya TCB na kutembelea mradi wa Reli ya Kisasa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salam – Morogoro katika jengo la Stesheni ya reli ya kisasa lililopo jijini Dar es salaam hivi karibuni Agosti, 2022.

Ziara ya menejimenti ya benki ya TCB imelenga kujionea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa SGR ili kudumisha uhusiano uliopo baina ya benki ya TCB na TRC.

Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa TCB imekua ikitoa fedha kwa TRC ili kuhakikisha miundombinu ya reli inaendelea kuwa maradufu hivyo benki hiyo imekua mdau mkubwa katika kuleta maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya reli nchini.

”TCB ni benki ya serikali na ni mdau muhimu sana sio tu kwa SGR, TCB ndio benki pekee iliyotuamini na kutupatia zaidi ya Bilioni 12 kipindi cha TRL, tunawashukuru sana” alisema Ndugu Kadogosa.

Pia Kadogosa alieleza kuwa kupitia mradi huo wa SGR benki zitapata fursa ya kuweka mashine za kutolea fedha (ATM) pamoja na ofisi katika stesheni zilizopo kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza hivyo ni vyema kuendelea kudumisha mahusiano baina ya TRC na mabenki.

“Tunakoenda tutahitaji maofisi zikiwemo benki pamoja na ATM ambazo wananchi wataweza kufanya miamala ya kuweka na kutoa fedha katika stesheni zetu za SGR” alisema Kadogosa.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu ameeleza kuwa mradi huo wa SGR una wakandarasi kwa awamu ya kwanza ambayo ina vipande vitano kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza hivyo fedha zilizotumika kutoka kwenye benki hiyo zimezaa matunda katika kuendeleza mradi wa SGR.

Naye Mwenyekiti wa Bodi kutoka benki ya TCB Dkt. Edmund Mndolwa alisema kuwa hatua iliyofanyika katika ujenzi wa mradi huo wa kimkakati ni kubwa kuanzia ujenzi wa stesheni hadi miundombinu ya reli pamoja na mifumo mbalimbali ya uendeshaji wa treni hiyo ya kisasa.

“Wananchi sasa wataweza kufanya kazi Dodoma na Kulala Dar es Salaam bila kupoteza muda safarini” alisema Dkt. Mndolwa.

Pia Mkurugenzi Mkuu wa benki ya TCB Ndugu Sabasaba Moshingi amesisitiza kuwa benki itaendelea kutoa ushirikiano wa kifedha kwa TRC ili kuhakikisha miundombinu ya reli nchini inaendeshwa kwa ufanisi ili uzidi kukuza uchumi wa nchi.

Shirika la reli nchini linaendelea kutoa fursa kwa wadau mbalimbali katika kuendeleza miundombinu ya reli na kushirikiana kibiashara kwa kusafirisha mizigo katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na nchi jirani.