Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

BEHEWA MPYA 44 ZATUA BANDARI YA DAR ES SALAAM, ZAPOKELEWA NA WAZIRI MBARAWA


news title here
06
October
2021

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amepokea Behewa mpya 44 za mizigo za Shirika la Reli Tanzania – TRC zilizonunuliwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati – TIRP, bandarini jijini Dar es SalaamOktoba 06, 2021.

Behewa hizo zitatumika kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaamhadi bandari kavu ya Isaka mkoani Shinyanga kwa kutumia reli ya zamani ambayo imefanyiwa maboresho kupitia mradi wa TIRP.

Pamoja na manunuzi ya Behewa mpya 44 za mizigo, mradi wa TIRP utaliwezesha Shirika la Reli Tanzania kupata vichwa vipya vya treni vitatu ambavyo viko katika hatua za mwisho za utengenezwaji wake ili viweze kuwasili nchini,

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amelitaka Shirika la Reli Tanzania kusimamia kwa weledi miradi yake inayolenga kuendeleza miundombinu ya reli akilenga mradi wa TIRP na ule waUjenzi wa Reli ya Kisasa - SGR ili kuimarisha uchumi wa nchi na kubadilisha maisha ya wananchi kwa ujumla kupitia huduma bora na za uhakika za usafiri na usafirishaji.

“Serikali imejipanga kuendeleza miundombinu ikiwemo reli, hii yote ni kuimarisha uchumi na kubadilisha maisha ya watu, kwahiyo tuitunze miradi kwa ajili yetu na vizazi vinavyokuja” alisema Prof. Mbarawa.

Aidha, Mheshimiwa Mbarawa ameihakikishia TRC kuwa Serikali itaendelea kutoafedha katika maboresho na ujenzi wa miundombinu ya reli na kulitaka Shirika lihakikishe linasimamia vyemawatendajimapato yapatikane kwa wingi na yatumike kununua behewa na vichwa vya treni.

“Serikali itaendelea kutoa pesa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya reli na TRC ina jukumu la kusimamia, Mkurugenzi na mwenyekiti hakikisheni mapato yanapatikana tununue behewa, vichwa na wananchi wapate huduma iliyo tukuka” alisema Mhe. Mbarawa

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro ameiomba Serikali iridhie tena kupitisha fedha zitakazotumika katika muendelezo wa maboresho ya reli ya kati awamu ya pili (TIRP 2) kwa kuwa mradi huu una umuhimu katika sekta ya usafirishaji wa reli.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bwana Masanja Kungu Kadogosa, ameeleza kuwa katika mradi wa Uboreshaji wa Reliya kati awamu ya kwanza (TIRP 1) ulijumuisha ununuzi wa behewa na vichwa, ujenzi wa Bandari kavu Isaka, ujenzi wa njia ya reli, madaraja na makalavti kutoka Dar es Salaam mpaka Isaka.

Halikadhalika, Mkurugenzi Mkuu Ndugu Masanja Kadogosa amebainisha kwamba katika mradi huo madaraja yameongezewa uwezo wa kupitisha mzigo ukilinganisha na wali ambapo madaraja mengi yalikuwa na uwezo wa kupitisha mzigo usiozidi tani arobaini (40) kwa behewa moja lakini kupitia maboresho hayo, madaraja hayo yanaweza kubeba tani 46 kwa behewa moja.

Kadogosa alimaliza kwa kusema kuwa, “Mheshimiwa Waziri mradi huu tulikuwa tumeagiza vichwa vitatu lakini hivi vichwa ni tofauti kidogo na vichwa tulivyonavo sasahivi vina ‘Horse Power 2000 -2100’ vichwa hivi vipya vina zaidi ya ‘Horse Power 3000’, maana yake ni kwamba sasa kutoka hapa kwenda Morogoro tutaweza kutumia kichwa kimoja badala ya viwili kuvuta behewa”