BANDARI KAVU YA ISAKA KURAHISISHA USAFIRISHAJI WA MIZIGO KWA NCHI JIRANI
September
2026
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeeleza dhamira ya kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo kwenda Bandari Kavu ya Isaka kwa kuongeza idadi ya treni na mabehewa, hatua inayolenga usafirishaji wa mzigo mkubwa kwa wakati mmoja.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Bandari Kavu ya Isaka, Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Bw. Jaffer Machano, amesema uwekezaji huo utawawezesha wafanyabiashara kutoka Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda kupata huduma za mizigo Isaka bila kulazimika kusafirisha magari hadi Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema Bandari Kavu ya Isaka ni sehemu ya mkakati mpana wa TRC wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa mizigo kupitia MGR na SGR, huku ujenzi na upanuzi wa vituo na bandari kavu nyingine ukiendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kwala, Morogoro, Isaka, Mwanza na Kigoma.
Mha. Machibya amesema TRC tayari imepokea ombi la kuongeza idadi ya treni kutoka kwa mwekezaji wa Bandari Kavu ya Isaka na itaendelea kuongeza treni kadiri kiwango cha mizigo kinavyoongezeka.
Naye Meneja wa Bandari Kavu ya Isaka kutoka GSM, Bw. Isack Kenyata alieleza kuwa ushirikiano kati ya serikali, TRC na sekta binafsi umeongeza kasi ya shughuli katika kituo hicho, ambacho kwa sasa kinahudumiwa na treni tatu kutoka Dar es Salaam, huku TRC ikiahidi kuongeza zaidi treni kulingana na ongezeko la mizigo.
TRC inaendelea kuimarisha reli kama kiungo muhimu cha biashara, uchumi na usafirishaji katika Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.

