Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

BANDARI KAVU YA ISAKA KUONGEZEWA UWEZO KUPITIA MRADI WA UBORESHAJI WA RELI YA KATI DAR - ISAKA


news title here
18
September
2019

Mradi wa Uboreshaji reli ya kati Dar - Isaka umepelekea kuongeza uwezo wa kupokea, kuhifadhi na kupakua mizigo Bandari Kavu ya Isaka, Uboreshaji huo unaendelea hivi sasa na matarajio ya kukamilika kwa mradi mwaka 2021.

Lengo la kuboresha bandari Kavu ya Isaka ni kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za usafirishaji mizigo kati ya Dar es Salaam, maeneo ya nyanda za Kaskazini na nchi jirani za Rwanda, Congo na Burundi ambazo zimekuwa zikitumia bandari kavu ya Isaka kusafirisha mizigo.

Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuboresha reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka yenye urefu wa KM 970. Reli hii ilijengwa zaidi ya miaka 100 na Mkoloni, ili kuleta ufanisi wenye tija kwa TRC, kuhakikisha uwepo wa usafiri wa uhakika, haraka na kuaminika wa treni utakaoziunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu ya Isaka.

Maafisa wanaondaa Gazeti la Reli na Matukio TRC walifika eneo ya Stesheni ya Isaka mkoani Shinyanga, eneo ambalo Mradi wa wa uboreshaji wa reli kati - TIRP unaishia kwa awamu ya kwanza na kuzungumza na Meneja Mradi wa TIRP kipande cha Itigi – Isaka Mhandisi Benard Mbonde ambaye amesema kuwa reli zilizopo eneo la Stesheni zinatarajiwa kurefushwa na kuongeza njia za kupishania ndani ya Bandari kavu, njia zitakazokuwa zikipitisha treni kwa ajili ya kupakua na kupakia mizigo hivyo eneo hilo litaweza kupokea treni nyingi zaidi za mabehewa ya mizigo.

Aidha Mhandisi Mbonde ameeleza kuwa kufunga njia kwa Saa 72 kumekuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa mradi huo kwani kasi ya uboreshaji imeongezeka, amesema kuwa kabla ya kupewa muda wa saa 72 kazi zilikuwa zikisuasua lakini mara baada ya kupewa muda wa saa 72 wameweza kufanya kazi kwa kasi kubwa na ufanisi.

“Nashukuru uongozi wa Shirika la Reli Tanzania, unaoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja zkungu Kadogosa kwa maamuzi ya busara na yenye kuleta tija kwa TRC na maslahi ya taifa".

Aliongeza kuwa "kabla ya kupata saa 72 wakandarasi walikua na uwezo wa kutandaza reli umbali wa Mita 200 pia katika uboreshaji wa tuta wakandarasi walikua wanasuasua, lakini baada kupata Saa 72 wakandarasi wameweza kuondoa reli ya zamani na kuweka reli mpya kipande cha zaidi ya Kilometa 30 na mpango wa saa 72 ulianza rasmi tarehe 12 Julai 2019, hivyo TRC imeweza kufanya kazi kubwa ndani ya muda mfupi” amesema Mhandisi Mbonde

Bandari kavu ya Isaka ilisajiliwa mwezi Septemba Mwaka 1999 kwa lengo la kuisogeza Bandari ya Dar es Salaam karibu na nchi za Rwanda, Burundi, DRC(Congo) na Uganda.

Kukamilika kwa Mradi wa uboreshaji wa reli ya kati kutawawezesha wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kwa haraka na kwa kiwango kikubwa kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Bandari kavu ya Isaka na hatimaye kwenda nchi jirani za Rwanda, Congo na Burundi.

Kutokana na haya yanayoendelea katika uboreshaji wa miundombinu ya Reli, TRC inawakumbusha watanzania kuendelea kuunga mkono Juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Jemedali, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika ulinzi wa miundombinu ya Reli kwa maana ya kuwa Reli hizi ni mali za watanzania na zinaboreshwa na kujengwa kwa fedha za watanzania .