Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BALOZI MAVURA ASHUHUDIA UTENGENEZAJI WA “TRENI ZILIZOCHONGOKA”, AWATOA HOFU WATANZANIA


news title here
26
July
2023

Balozi wa tanzania nchini Korea ya kusini Mhe. Togolani Mavura ametembelea kiwanda cha kampuni ya Hyundai Rotem na kukagua maendeleo ya utengenezaji wa seti 10 za treni za kisasa na vichwa 17 vya treni vya umeme mjini Changwon, Korea ya kusini Julai 26, 2023.

Akiwa katika karakana inayotengeneza seti za treni za kisasa (EMU) Balozi Mavura ameeleza kuridhishwa na kazi iliyofanyika mpaka sasa na kuwatoa hofu watanzania juu ya maendeleo ya utengenezaji wa vifaa hivyo vitakavyotumika katika reli ya kisasa SGR nchini.

“Kazi ni nzuri na hizi ndio picha ambazo watanzania wengi walikuwa na Shauku ya Kuziona, nimefanikiwa kuona eneo la ndani, kilichonivutia Zaidi ni kuwa treni hizi zimezingatia watu wenye ulemavu mfano katika eneo la maliwato, pia kuna eneo maalum la akina mama kuwahudumia Watoto kwahiyo itatubadilishia namna ya kusafiri na itatoa uhuru kwa kila mtu kusafiri, kwahiyo nimpongeze Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoahidi na kweli kazi hii inaendelea” alisema Balozi Mavura.

Aidha Balozi Mavura amesema kuwa biashara kati ya Tanzania na Korea ya kusini imeimarika zaidi kutokana na makampuni ya nchi hiyo kuhusika katika shughuli za ujenzi wa reli na utengenezaji wa vifaa vya uendeshaji wa reli ya Kisasa.

“kwa kununua vifaa hivi vya uendeshaji, kiwango cha biashara kati ya nchi zetu mbili kimepanda kwa 1.4%, tumenunua vifaa lakini pia na wao wametuuzia teknolojia”.

Kwa upande wake Mhandisi Kelvin Kimario, meneja mradi wa ununuzi wa vifaa hivyo ameeleza kuwa watanzania wanapaswa kutofautisha vichwa vya treni vya umeme na seti za treni za kisasa (EMU).

“kichwa kinakuwa na uwezo wa kuvuta mabehewa ya abiria au ya mizigo na kinajitegemea katika uendeshaji lakini kwa upande wa seti za treni za kisasa, hizi zinakuwa ni seti, seti moja inaweza kuwa na vipande sita mpaka nane vinavyotegemeana katika uendeshaji na kwasababu hiyo haviwezi kutenganishwa vinafanya kazi kwa Pamoja” alisema mhandisi Kimario.

Kabla ya kutembelea eneo zinapotengenezwa seti za treni za kisasa Balozi Mavura alikagua kimoja kati ya vichwa vya treni vya umeme, kilichokamilika na kushuhudia kikitembea katika reli katika eneo maalum la majaribio ya uendeshaji.

Wakati vichwa viwili vya treni vya umeme vikitegemewa kuingia nchini hivi karibuni kutoka ujerumani, kampuni ya hyundai rotem inatarajia kuanza majaribio ya kiwandani ya seti za treni za kisasa mwishoni mwa mwaka huu.