Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​AWAMU YA PILI YA KAMPENI YA UELEWA KWA JAMII KUHUSU SGR


news title here
10
October
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na awamu ya pili ya Kampeni ya Uelewa kwa jamii kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR kipande cha Mwanza – Isaka katika mkoa wa Shinyanga na baadaye kuifikia mikoa ya Mwanza na Simiyu, Oktoba 2022.

Katika awamu hii ya kampeni jumla ya vijiji 73 vinavyopitiwa na mradi katika wilaya nane za mikoa hiyo, vinatarajiwa kufikiwa lengo likiwa ni kuwashirikisha viongozi, wananchi na wadau katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ili kuleta uelewa sawa juu ya masuala mbalimbali yanayouhusu mradi.

Ujumbe wa kampeni hii unaojumuisha wataalamu kutoka idara mbalimbali za Shirika la Reli Tanzania, unatilia mkazo masuala ya kijamii, afya, utunzaji wa mazingira, fursa za kiuchumi zitokanazo na mradi pamoja na ulinzi na usalama wa mali za mradi na miundombinu ya reli.

Afisa kutoka kitengo cha usimamizi wa masuala ya kijamii cha Shirika la Reli Tanzania, kinachoratibu kampeni hiyo Bi. Tumaini Rikanga, amesema kuwa licha ya kufanyika kwa zoezi kama hili kabla ya kuanza kwa shughuli za ujenzi, awamu hii ya kampeni ya uelewa inawapa fursa zaidi wananchi na viongozi kuelewa kwa kina masuala mbalimbali kutokana na kuwa shughuli za ujenzi wa mradi zinaendelea katika maeneo yao.

“Utofauti ni kwamba katika awamu hii ya pili ya kampeni ya uelewa, unaposema reli hii ya kisasa ni tofauti na ile ya zamani, wanaelewa hata kwa kutazama tuta la reli linalojengwa lakini pia hata unaposema tutajenga vivuko maalumu, wanapata picha halisi kwakuwa maandalizi ya ujenzi wa vivuko hivyo yameshaanza” aliongeza Bi. Tumaini.

Aidha, Bi. Tumaini amesema kuwa katika zoezi hili lililoanza tarehe 3 Agosti, 2022 tayari jumla ya vijiji 12 katika wilaya ya Shinyanga Vijijini vimefikiwa na kuwa kampeni itafanyika pia katika wilaya za Shinyanga Manispaa, na KIshapu mkoani humo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyashimbi mkoani Shinyanga Bi. Cecilia Maganga, amesema kuwa elimu inayotolewa katika mikutano hiyo ni muhimu katika kurahisisha kazi ya viongozi katika vijiji.

“Elimu hii inawasaidia wananchi wetu kuelewa hata mipaka kati yao na mradi pamoja na kufahamu umuhimu wa kutoingilia mipaka hiyo, kazi hii ingekuwa ngumu sana kwetu wenyeviti na watendaji kwani hata sisi tusingeelewa chochote” alisema Bi. Cecilia.

Awamu ya pili ya kampeni ya Uelewa kwa jamii kuhusu ujenzi wa SGR Mwanza – Isaka inafanyika wakati ambapo maendeleo ya ujenzi wa mradi yakiwa yamefikia zaidi ya 14% ambapo kazi za ujenzi wa madaraja, makaravati, vivuko na tuta la reli zikiendelea katika kipande chote chenye jumla ya Km 341.