ABIRIA ZAIDI YA MILIONI 2.3 WASAFIRI NA SGR; MAKUSANYO YAFIKIA BILIONI 66.8

May
2025
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa TRC imeweza kusafirisha zaidi ya abiria milioni 2.3 tangu kuanzishwa kwa uendeshaji wa treni ya SGR June 14, 2024 hadi sasa Aprili, 2025.
Akizungumza katika kipindi cha " One on one" cha Wasafi TV Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa tangu kuanzia kwa uendeahaji wa treni ya mwendokasi, wananchi na abiria wameitikia kwa wito mkubwa katika utumiaji wa usafiri wa treni tangu kuanza June, 2024 hadi kuzinduliwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Jijini Dodoma Agosti 1, 2025 kutoka Dar es salaam, Morogoro hadi Dodoma.
"Hadi kufikia Aprili 2025, TRC imeweza kusafirisha zaidi ya abiria milioni 2.3 na mapato yaliyopatikana katika uendeshaji yamefika takribani bilioni 66.8 kwa mkoa wa Dar es salaam, Morogoro na Dodoma" amezungumza Mkurugenzi mkuu TRC Masanja Kadogosa.
Aidha, Mkurugenzi mkuu ameeleza kuwa kadri siku zinavyosonga uhitaji mkubwa wa matumizi ya treni iendayo haraka unaongezeka kwa kasi. Kwa upande huo huo imechochea kuongezeka na kubadilika kwa ratiba za uendeshaji wa treni hizo kwa safari za siku nzima kwa treni ya mwendokasi, kwa mkoa wa Dar es salaam, Morogoro, na Dodoma.
" Safari za Morogoro hadi Dar es salaam zinajitegemea ikiwa na treni ya peke yake inayokwenda na kurudi mara mbili kwa siku ikiwa na ratiba ya safari nne kwa siku pia uhuitaji na wingi wa abiria umepelekea TRC kuongeza treni ya Dar es salaam hadi Dodoma kuwa na jumla ya treni nne ambazo zinakwenda na kurudi kwa siku mara mbili kwa safari nane kwa siku" ameeleza Masanja Kadogosa Mtendaji Mkuu TRC
Katika hatua nyingine, Ndugu Kadogosa amezungumza kuwa TRC katika nyakati za matatizo hasa ya kiufundi katika uendeshaji wa treni ziendazo kasi imekuwa ikifanya kwa ueledi na ufanisi mkubwa kuhakikisha inatatua changamoto inayojitokeza kwa wakati husika , pamoja na hayo ametoa pongezi kwa vijana wanaoshughulika na kutatua changamoto hasa za kiufundi, kwani wanafanya kazi kubwa kuhakikisha uendeshaji unakuwa katika hali ya usalama.
" Ikumbukwe kuwa hatujawahi kua na treni ya nishati ya umeme, hivyo vijana wanafanya kazi kubwa sana, hata hivyo katika Afrika ya Mashariki na Kati hakuna nchi yeyote iliyothubutu kuendesha yenyewe treni za aina ya mwendokasi, ila sisi tunafanya wenyewe uendeshaji wa treni" aliongezea Ndugu Masanja Mkurugenzi mkuu TRC.
Aidha Ndugu Kadogosa alifafanua awamu ya kwanza ya mradi ambayo ina vipande vitano, ambapo kipande cha kwanza ni kuanzia Dar es salaam hadi Morogoro, cha pili Morogoro hadi Makutupora ya Singida, cha tatu Makutupora hadi Tabora 15%, cha nne Tabora hadi Isaka 6.87% na cha tano ni Isaka hadi Mwanza 63%, vilevile awamu ya pili ya ujenzi ni kuanzia Tabora hadi Kigoma 7.88%, Uvinza hadi Musongati.
Shirika la Reli Tanzania linaendelea na usimamizi wa ujenzi wa vipande vilivyobaki kujengwa kwa ufanisi na kuhakikisha vinaisha kwa wakati kama mkataba wa ujenzi wa SGR unavyoeleza ambapo kipande cha Dar es salaam hadi Mwanza usafirishaji utaanza 2027, na Tabora hadi Kigoma usafirishaji kuanza baada ya kukamilika 2028.