Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​408 WAHITIMU KATIKA MAHAFALI YA TATU YA TIRTEC


news title here
09
December
2023

Wahitimu 408 wamehitimu mafunzo ya ngazi ya Stashahada, Astashahada ya Awali na Astashahada katika Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania – TIRTEC katika mahafali yaliyofanyika mkoani Tabora, Disemba 8, 2023.

Katika mahafali ya tatu ya TIRTEC jumla ya wahitimu 408 wamefaulu masomo katika kada mbalimbali ikiwemo matengenezo ya njia, matengenezo ya vichwa na mabehewa na usafirishaji katika reli. Wahitimu wa kozi katika ngazi ya Astashahada ya Awali ni 343, Astashahada ni 11 na Stashahada ni 54.

Mahafali yamehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo Cha Teknolojia ya Reli Tanzania Mhandisi Alfred Nkinda Ng‟hwani, Wajumbe wa Bodi ya Chuo, Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bi. Amina Lumuli, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora Bi. Asha Churu, Wakufunzi, wafanyakazi wa Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania na wafanyakazi wote wa Shirika la Reli Tanzania.

Mgeni rasmi katika mahafali ambaye ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Bwana Juma Japhet Kaponda amesema kuwa kuhitimu katika fani yoyote ni matokeo ya jitihada za muda mrefu pamoja na michango ya hali na mali kutoka kwa walimu, wazazi na walezi.

Pia Bwana Kaponda ameipongeza menejimenti ya Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania kwa kuendesha shughuli mbalimbali za kuendeleza taaluma ya Teknolojia ya Reli kwa weledi wa hali ya juu kupitia ubunifu katika kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuandaa wataalamu wa sekta ya reli nchini.

“Nafahamu na napenda kusema mbele ya wageni waliopo hapa kwamba Chuo Cha Teknolojia ya Reli Tanzania ni chuo pekee Tanzania kinachotoa wahitimu mahiri na wenye maadili ya kazi katika idara zote zilizopo katika Shirika la Reli Tanzania” aliongeza Bwana Kaponda

Mkuu wa Chuo cha TIRTEC Bwana Daniel Mwajanga ameeleza kuwa “Chuo kina miundombinu muhimu ambayo inasaidia katika kutoa elimu stahiki kwenye sekta ya usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya reli. Miundombinu iliyopo ni madarasa ya kufundishia, Karakana za uhandisi mitambo, Uhandisi wa mtandao wa mawasiliano na umeme, Maabara ya tarakilishi (Kompyuta), maktaba ya Chuo yenye tarakilishi (kompyuta) zinazounganishwa na mfumo wa mtandao uliojengwa na Shirika la Reli Tanzania katika miundombinu ya chuo pamoja na kuwepo kwa vitabu vya ziada na kiada ili kuwarahisishia wakufunzi na wanafunzi kupata huduma nzuri za kitaaluma.

Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania kinasimamiwa na Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania kwa lengo la kuzalisha wataalamu watakaofanya kazi katika shughuli mbalimbali za uendeshaji wa huduma za usafiri wa reli. Kupitia mahafali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bi. Amina Lumuli alipata fursa ya kusikiliza maombi na changamoto zinazokikabili Chuo cha Reli na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutatua changamoto zilizopo.

Bi. Amina alieleza kuwa Serikali kupitia Shirika la Reli iko kwenye mpango wa kuboresha Chuo cha Reli kwa kujenga majengo mapya ya chou kitakachokuwa na miundombinu wezeshi kwaajili ya kusomea na kufundishia.

“Menejimenti ya Shirika la Reli inaendelea kuhakikisha kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha miundombinu ya chuo inakarabatiwa kwa mpango wa muda mrefu na mfupi na kuweka mazingira mazuri na salama kwaajili ya kufundishia na kujifunzia, miundombinu bora itakiwezesha Chuo kutoa wataalamu wenye umahiri wa kutosha kwenye taaluma hii ya reli fanyiwa” alisisitiza Bi. Amina