141 WAHITIMU CHUO CHA RELI, TRC YAANIKA MIPANGO UPANUZI WA CHUO

December
2022
Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania, TIRTEC kimefanya mahafali yake ya pili ambapo jumla ya wahitimu 141 wametunukiwa vyeti, astashahada ya awali na astashahada katika taaluma mbalimbali za sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli, Disemba 10, 2022 mkoani Tabora.
Mahafali hayo yamefanyika katika viwanja vya chuo hicho mkoani Tabora ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Katibu tawala wa mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya ambae amemuwakilisha mkuu wa mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Mboya ameupongeza uongozi wa chuo kwa kuwaandaa vyema vijana hao ambao mabali na shughuli za kitaaluma, wameshiriki katika shughuli mbalimbali za ukarabati mdogo chuoni hapo.
Aidha Dkt. Mboya ameongeza kuwa “endeleeni kutafuta ujuzi wa juu zaidi kwani elimu haina mwisho, ili shirika na taifa kwa ujumla liwe na wataalamu wa reli wenye kuleta tija kwa uchumi wan chi yetu”
Dkt. Mboya ameeleza kuwa chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania na Shirika la reli ni kichocheo muhimu katika kulifanya taifa kuifikia dhana ya uchumi shindani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu na utawala, Bi. Amina Lumuli akimuwakilisha mkurugenzi mkuu wa TRC, amesema kuwa shirika lipo katika mpango wa kukarabati na kukipanua Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania ambapo utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR kipande cha Makutupora – Tabora na Tabora Isaka, aidha shirika pia limedhamiria kufanya ukarabati wa majengo katika kampasi ya Morogoro.
“ukarabati wa chuo kwa hapa Tabora utaanza hivi karibuni, pia katika utekelezaji wa kipande cha nne cha mradi, tutajenga majengo mapya ya chuo, tuna eneo la kilomita za mraba 740,579 na majengo hayo yatakuwa ya kisasa pamoja na mabara za kisasa kuendana na kasi ya teknolojia ya uendeshaji wa Reli” aliongeza Bi. Amina Lumuli.
Naye Edina Msalenge, mhitimu pekee wa kike katika orodha ya wanafunzi waliofanya vizuri kwa kila kozi amewataka wasichana kote nchini kuweka bidii katika masomo na kuwahimiza kuchangamkia fursa katika taaluma zinazoaminika kuwa ni za kiume.
Udahili wa wanafunzi katika chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka tangu 2016 kilipopata ithibati ambapo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 wanafunzi 381 ambalo ni ongezeko la 20% ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2021/2022.