Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAZINDUA MAFUNZO YA HUDUMA KWA WATEJA


news title here
06
November
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii wamefungua mafunzo ya siku 14 kwa wafanyakazi 70 wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR awamu ya kwanza yenye kauli mbiu ''HAKIKISHA MTEJA ANARUDI'', mafunzo yanafanyika katika Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 06 Novemba 2023.

Mafunzo yanahusisha maafisa mbalimbal ikiwemo stesheni masta, wakatisha tiketi, maafisa usafirishaji, watoa huduma kwa wateja na maafisa biashara.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli amesema mafunzo yatasaidia kuwapa uwezo wafanyakazi kutoa huduma bora za kiwango cha kimataifa kwa abiria.

"Chuo hiki cha utalii wa Taifa kimekasimiwa kutoa mafunzo haya ikiwemo mafunzo ya ukarimu na huduma kwa wateja kwahiyo wafanyakazi watapata mafunzo bora na kwa kuisadiana na menejimenti tutaenda kutoa huduma bora kwa abiria wetu wa ndani na nje ya nchi watakaotumia usafiri wetu" ameongeza Bi. Amina Lumuli.

Pia Bi. Amina Lumuli amesema mafunzo yatasaidia wafanyakazi namna ya kuwasiliana wenyewe kwa wenyewe wawapo kazini pamoja na kuwasiliana na wateja katika kiwango cha kimataifa ili kukidhi huduma bora.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Bi. Jesca William amesema watahakikisha watoa huduma kwa wateja pamoja na kada zingine zinazoshiriki mafunzo wanapata ujuzi wa kuhudumia wateja ikiwemo kuzingatia mazingira ya mteja ili kuhakikisha mteja anarudi kusafiri na treni za kisasa.

"Mafunzo haya ni chachu ya kuongeza biashara na kuweza kuvuta wateja wengine waweze kuhudumia na Shirika la Reli Tanzania kupitia treni za reli ya kisasa - SGR ambazo zinaenda kuanza kutoa huduma nchini". amesisitiza Bi. Jesca William.

Afisa usafirishaji Mwandamizi wa TRC Bi. Edna Hezron ambae ni mshiriki wa mafunzo ya mtoa huduma kwa wateja amesema kupitia mafunzo watapata ujuzi katika utoaji wa huduma ndani ya treni na katika stesheni zote.

"Niwahakikishe wateja wetu kua huduma ambazo tutazitoa ni huduma bora Bora za kiwango cha kimataifa na tutaenda kutoa huduma kwa kupitia kauli mbiu ya "HAKIKISHA MTEJA ANARUDI" , ameongeza Bi Edna.

Naye Afisa Biashara Msaidizi Bw. Denis Otaru kutoka TRC amesema elimu na ujuzi watakaoupata kwenye mafunzo itawawezesha kuhudumia wateja wa ndani na nje ya nchi kwa kutoa huduma stahiki za kimataifa kwa wateja wote, mafunzo haya yatasaidia kuendeleza na kuboresha mradi kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.

TRC imepewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa katika awamu ya kwanza Dar es Salaam - Mwanza na awamu ya pili Tabora - Kigoma, TRC inatarajia kuanza majaribio ya treni ya umeme hivi karibuni katika kipande cha kwanza Dar es Salaam hadi Morogoro.