Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAFANYA SEMINA KWA WAFANYAKAZI WANAOSIMAMIA SGR


news title here
06
August
2023

TRC YAFANYA SEMINA KWA WATUMISHI WANAOSIMAMIA UJENZI WA SGR

Shirika la Reli Tanzania - TRC limefanya semina ya siku mbili ya maadili kwa watumishi wanaosimamia ujenzi wa mradi wa Reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR katika ukumbi wa bandari jijini Dar es Salaam, Agosti 2023.

Semina hiyo imehusisha watumishi wa reli wanaosimamia ujenzi wa mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa awamu ya kwanza wakiwemo mameneja na wasaidizi wao, maafisa jamii, maafisa mazingira na maafisa ardhi kutoka TRC.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Bi. Amina Lumuli amesema lengo la mafunzo ni kutoa uelewa na kufuata Sheria na taratibu za maadili za Utumishi wa Umma kwa wasimamizi wa miradi na watumishi wa kada mbalimbali zinazohusika na ujenzi na mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR katika awamu ya kwanza ambayo ni Dar es Salaam hadi Mwanza na awamu ya pili Tabora - Kigoma.

Watoa mada katika semina walikua maafisa kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, TAKUKURU na Idara ya Usalama wa Taifa.

"Tunajua kwamba mradi huu unajengwa kwa gharama kubwa kwahiyo wasimamizi wa mradi leo wamepata elimu kutoka TAKUKURU dhidi ya Rushwa wawapo maeneo ya kazi sababu wanaweza kushawishika kwa namna moja au nyingine" ameongeza Bi. Amina Lumuli.

Afisa Masuala ya Jamii Bi. Tumaini Rikanga amesema kupitia semina hii amejifunza namna mtumishi wa Serikali anavyopaswa kufuata Sheria na kanuni za kazi katika utendaji kazi na kuhudumia jamii kwenye eneo lake la kazi.

TRC imeaminiwa na Serikali katika kusimamia ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR katika awamu ya kwanza Dar es Salaam - Mwanza na ujenzi wa awamu ya pili Tabora hadi Kigoma ambao umeanza katika hatua za awali.