Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

ZOEZI LA ULIPAJI WA FIDIA KUPISHA UJEZI WA SGR MOROGORO – MAKUTUPORA LAZIDI KUPAMBA MOTO JIJINI DODOMA


news title here
03
August
2020

Shirika la reli Tanzania linaendelea na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wakazi wa jiji la Dodoma ambao maeneo yao yalitwaliwa na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR kipande cha pili kutoka Morogoro,Dodoma hadi Makutupora hivi karibuni Agosti 2020.

Katika zoezi hilo la siku 15, jumla ya wakazi 872 kutoka maeneo tofauti tofauti ya jiji hilo watalipwa fidia zao na tayari mpaka sasa limefikia siku 13 tangu lilipoanza Julai 23,2020,ambapo limefanyika katika hali ya kuridhisha kwani kiasi kikubwa cha wakazi wanaostahili fidia wamekwisha kabidhiwa hundi zao.

Afisa uhasibu kutoka shirika la reli Tanzania,TRC Bw. Nassor Ramadhani Said,amesema kuwa zoezi limeenda vizuri na kuwa ni kiasi kidogo tu cha wananchi wanaostahili kulipwa katika awamu hii,wamesalia.

“Tumepiga hatua kubwa mpaka sasa ambapo ni siku ya 13 na watu 788 tayari tumeshawalipa kwahiyo katika hizi siku mbili tutakamilisha kwa hao watu zaidi ya mia moja waliobaki” alisema Bw.Nassor.

Aidha kuhusu wananchi ambao wamekwisha fanyiwa uthamini wa maeneo yao lakini bado hawajalipwa fidia,Bw.Nassor amesema kuwa hakuna mwananchi ambae eneo lake lilitwaliwa na mradi, hatalipwa.

“sisi tumeaminiwa na serikali kufanya hii kazi kwahiyo hatuwezi kwenda nje na makubaliano kwasababu kama maeneo tuliyatwaa lazima tulipe fidia,na kama wanavyoona tumeanza kuwalipa na tunakaribia kuwamaliza”

Baadhi ya wanachi ambao tayari wamekwisha lipwa fidia zao wameelezea kufurahishwa na zoezi hili na kueleza shukurani zao kwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mzalendo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Mmoja kati ya wananchi ambao wamelipwa fidia katika awamu hii, Bi.Vickless Pius amesema “nipende tu kuishukuru Serikali kwa kutuletea huu mradi,maana mradi umeleta maendeleo kwenye kata yetu na utakapokamilika itakuwa rahisi na haraka kwa sisi wafanyabiashara kusafiri kati ya Dodoma na Dar es Salaam”

Kwa siku 12 zoezi hilo limefanyika katika kata ya Ihumwa na limehamia katika ofisi za Shirika la reli Tanzania TRC, eneo la stesheni ya Dodoma ili kutoa nafasi ya kuwalipa wananchi wa maeneo mengine ya Mkoani Dodoma ambao pia maeneo yao yalitwaliwa na mradi.