Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​ZAIDI YA ASILIMIA 77 YA WANANCHI WALIPWA FIDIA KUPISHA MRADI WA SGR TABORA HADI MWANZA


news title here
17
February
2025

Shirika la Reli Tanzania - TRC limelipa fidia zaidi asilimia 77 ya wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa ili kupisha Ujenzi wa mradi wa SGR Kipande cha nne Tabora - Isaka na kipande cha tano Isaka - Mwanza hivi karibuni Februari, 2025.

Timu kutoka TRC ikiongozwa na Afisa Ardhi kutoka - TRC Bw. Ramadhani Mfikilwa ameeleza kuwa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliotwaliwa ardhi ni zoezi enendelevu hadi pale mradi utakapokamilika na kusema kuwa TRC inahakikisha kila muhusika anapatiwa stahiki zake kwa kufuata taratibu zilizowekwa na serikali.

" 77.59% wamelipwa, 7.47% hawajalipwa na 14.94% ni maeneo ya Serikali ya Vijiji ambayo hayalipiwi fidia, mfidiwa lazima awe anatambulika na kiongozi wa kijiji ama mtaa kwa kukabidhiwa barua sambamba na nyaraka alizopatiwa wakati wa uthamini” alieleza Afisa Ardhi - TRC Bw. Ramadhani Mfikilwa.

Kwa upande mwingine, Bw. Ramadhani Mfikilwa alisema kuwa hundi wanazopatiwa wafudiwa hukaa kwa muda wa ukomo wa miezi sita na hivyo hata muda wa matumizi ya hundi utakapofika kikomo bado TRC itaandaa hundi nyingine za malipo kwa wahusika watakaopatikana ili kulipwa stahiki zao.

Aidha Bw. Mfikilwa ameeleza kuwa TRC itaendelea kutwaa ardhi na maendelezo yaliyoko juu ya ardhi endapo kutakuwa na uhitaji wa maeneo pia kuwaasa wananchi kushirikiana na TRC kuwa mstari wa mbele katika kutoa maeneo yao kwaajili ya maslahi ya maendeleo ya wananchi na nchi kiujumla" ameeleza Afisa Ardhi - TRC Bw. Ramadhani Mfikilwa.

Naye Meneja wa Biashara kutoka Benki ya Taifa ya Biashara - NBC Bw. Regan Daud wa tawi la Shinyanga amezungumza kuwa, NBC ni wadau wakubwa wa TRC hivyo NBC imeshiriki vyema katika zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopitiwa na mradi. Aidha NBC inahakikisha inamfungulia mnufaika akaunti kwa haraka ili kuwekewa fedha na TRC kupitia akaunti.

" Sisi kama taasisi ya kifedha na wadau wakubwa wa TRC, tupo hapa kurahisisha huduma za ulipaji fidia inayofanyika kwa njia ya hundi hivyo wanufaika tunawafungulia akaunti za NBC ili kupata malipo kwa urahisi" ameeleza Bw. Regan Daud Afisa Biashara - NBC tawi la shinyanga.

Pia Mkazi wa Kijiji cha Muhida Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Bw. Mathayo Gwisu amesema kuwa, muda mrefu umepita tangu maeneo yatwaliwe kupisha Ujenzi wa mradi wa SGR, watu walihisi hawatalipwa fidia za maeneo lakini zoezi la ulipaji fidia linaendelea katika kijiji cha Muhida, wanufaika wanalipwa stahiki zao.

" Serikali haijasahau stahiki ya mtu, ndiyo maana leo tumefikiwa katika kijiji chetu ili kulipwa fidia za maeneo yetu yaliyotwaliwa" ameeleza Bw. Mathayo Gwisu.

Bw. Robert Mwigonji Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Goloma Kata ya Mandu Mkoani Mwanza ameongezea kuwa, Mradi wa SGR utakapokamilika utaletafaida katika kijiji cha Goloma ikiwa uchumi na shughuli za kimaendeleo, biashara zitakua kupitia usafirishaji wa mizigo kwa urahisi ndani ya nchi, wananchi wamepisha maeneo ili kuwezesha Ujenzi wa mradi wa kimkakati unafanyika kwa ubora kama stadi za mradi zilivyoelekeza.

" Leo tumefikiwa na ugeni kutoka TRC kwa ajili ya kulipa wananchi fidia kwenye maeneo ya makaburi ambayo yamepitiwa na mradi wa SGR, zoezi limeenda vizuri kila mmoja amepewa hundi yake" alisema Bw. Robert Mwigonji Afisa Mtendaji Goloma

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea kusimamia vyema Ujenzi wa mradi wa reli ya kimkakati ya SGR kwa awamu ya kwanza Kuanzia Dar es salaam hadi Mwanza na awamu ya pili kuanzia Uvinza Tanzania hadi Musongati nchini Burundi, ili kupanua na kukuza mawanda mapana ya ukuaji wa uchumi, kijamii na maendeleo makubwa ya biashara.