WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO MHANDISI ISACK KAMWELWE AFUNGUA RASMI KAZI YA UUNGAJI RELI YA KISASA - SGR.
April
2019
Waziri wa ujenzi uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe afungua rasmi kazi ya kuunganisha Reli ya kisasa - SGR nje kidogo ya kambi ya SGR ya Soga Kibaha hivi karibuni 2019.
Mhe. Waziri Kamwelwe azindua rasmi kazi ya kuchomea Reli ya kisasa - SGR kwa lengo la kuunganisha na kuondoa maungio yote kwenye Reli.
Kuunganishwa kwa Reli hupunguza msukosuko kwa abiria na mizigo, kuleta uimara wa njia na kupunguza uharibifu wa njia.
Aidha Waziri Kamwelwe aliongezea kuwa Ujenzi wa reli ya kisasa - SGR unakwenda vizuri kwa kuwa kazi inaonekana na inakwenda kwa kasi nzuri.
Amesema Waziri Kamwelwe "kama mnavyoona vifaa viko hapa tumefikia hatua ambayo inaonekana, tuta limeshajengwa, mataruma yamewekwa na reli imewekwa, leo nimezindua kuunganisha reli kwa umeme bila kutumia 'material' mengine yoyote, uungaji huu umefanyika mara ya kwanza Tanzania, reli hii itakuwa ni moja kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora"
Waziri Kamwelwe ameongeza kuwa serikali imewapa kipaumbele @wahandisi na mafundi watanzania katika mradi pamoja na kuendesha mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa kuna wataalam wa kutosha.
Amesema Kamwelwe “Tumeweka watumishi watanzania wa kutosha, tuna wahandisi wa umeme, ujenzi, mafundi wa kuchomelea ili kila mmoja ajifunze kitu kipya na bado tunaendelea kupeleka watumishi nje ya nchi kujitunza".
Hafla ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa, Wafanyakazi TRC, wanahabari pamoja na wananchi wa Soga Kibaha mkoani pwani.