Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAZIRI MBARAWA AJIONEA MAANDALIZI YA TRC KUELEKEA MVUA ZA EL NIÑO


news title here
08
October
2026

Morogoro, Oktoba 6, 2026 – Wizara ya uchukuzi imelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kuchukua hatua za tahadhari na kufanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha usalama wa abiria, mizigo na miundombinu ya reli wakati wa msimu unaotarajiwa wa mvua za El Niño.

Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua na kujionea utayari wa TRC katika maeneo ya Kilosa, Gulwe, Kidete na Godegode Mkoani Morogoro, kujiandaa kwa lengo la kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

Katika maeneo hayo, TRC inaendelea kutekeleza kazi mbalimbali za kuimarisha na kulinda miundombinu ya reli, ikiwemo kujenga uzio katika kingo za Mto Mkondoa na maeneo ya makorongo, kuondoa mchanga na vifusi ndani ya mito, kuboresha madaraja ili kuongeza uwezo wa kupitisha maji mengi bila kuathiri kingo za mito, pamoja na kuweka mawe makubwa katika kingo za mito na makorongo ili kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kulinda miundombinu ya reli.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhe. Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa TRC kujiandaa mapema na kufuatilia kwa karibu hali ya miundombinu na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza madhara yatokanayo na mvua hizo.

Aidha, amelitaka Shirika kuhakikisha huduma za usafiri wa reli zinaendelea kutolewa kwa usalama na ufanisi, huku likizingatia zaidi usalama wa abiria na mizigo pamoja na ulinzi wa miundombinu ya reli.

Utayari huo wa TRC, ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha miundombinu ya reli inaendelea kuwa imara na huduma za usafiri wa abiria na mizigo zinaendelea kama kawaida lakini kwa usalama katika kipindi cha msimu wa mvua tarajiwa za El Nino.