Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WASANII, WAANDISHI WA HABARI WATEMBELEA MRADI WA RELI YA KISASA DAR - RUVU


news title here
16
October
2020

Wasanii wa tasnia mbalimbali pamoja na waandishi wa habari wamepata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Ruvu mkoani Pwani ambapo wameongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abasi, Oktoba 16, 2020.

Katika ziara hiyo Wasanii na Wanahabari wamepata kujifunza mambo mbalimbali katika mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa na kuona njia za juu na za chini ambazo itapita treni ya kisasa, vivuko vya watu na mifugo, majengo ya stesheni ikiwemo stesheni kubwa ya Dar es Salaam, Pugu, Soga na Ruvu.

Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa wasanii watapata fursa ya kuzidi kujitangaza na kufanya kazi zao za sanaa kupitia mradi huo wa reli ya kisasa pindi utakapokamilika pamoja na fursa za kuanzisha biashara mbalimbali katika stesheni kubwa za reli ya kisasa ikiwemo ya Dar es salaam kwa kuwa na maeneo makubwa ya kufanyia biashara.

Aidha, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa kupitia ziara hii wamejifunza na kujiona kwa macho maendeleo ya nchi kupitia mradi mkubwa Afrika Mashariki na wao kama vioo wa jamii watapata nafasi ya kuwapa mafunzo wananchi juu ya maendeleo ya mradi huo.

"Ziara hii ina umuhimu mkubwa sababu wakijifunza hawa watapeleka mafunzo pia kwa jamii" aliongezea Dkt. Abbasi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa mradi wa SGR utakua na faida kubwa sana kwa nchi na wananchi kwa kunufaika katika mambo ya usafirishaji wa watu na mizigo na pia faida za ufanyaji wa kibiashara na ajira.

Hata hivyo Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa wasanii na waandishi wa habari wamekua kipaumbele katika kutangaza mambo yanayoleta maendeleo ya nchi na pia wanaendelea kujifunza na kuzidi kutangaza mambo makubwa yanayofanywa na Serikali.

Msanii wa muziki Mrisho Mpoto amesema kuwa wasanii wanapaswa kuwa mabalozi kwa kuitangaza nchi kupitia ziara waliyoifanya ambayo wamepata kuona mambo makubwa katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa na pia kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwa utekelezaji pia kuiomba TRC kuendelea na juhudi za kusimamia mikakati na kazi zote zinazofanyika katika mradi huo wa SGR.

“Kiukweli imetusisimua kwa mradi huu kujengwa na fedha zetu, kodi zetu sisi wenyewe“ alieleza Mpoto.