Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WILAYANI UYUI,URAMBO WAASWA KUWAJIBIKA KULINDA MIUNDOMBINU YA RELI


news title here
02
April
2025

Wananchi wa wilaya ya Uyui na Urambo Mkoani Tabora wameaswa kuwajibika kulinda miundombinu ya reli kwenye kipande cha sita cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) Tabora - Kigoma.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Kikosi cha Reli (ACP) Venance Mapala, kwenye kampeni jumuishi ya jamii juu ya masuala ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli na kuwa na wajibu wa kila mmoja kumlinda mwengine.

“Serikali itashughulika na kuwasaka wahalifu popote pale walipo na wananchi wanatakiwa kutoa taarifa pale wanapoona kuna uhalifu unatokea na sheria itawalinda ya mwenendo wa makosa ya jinai Sura ya 16 ambayo inampa mamlaka kila mtu ana uwezo wa kumkamata mhalifu pale ambapo ataona uhalifu unafanyika mbele yake” alizungumza ACP Mapala.

ACP Mapala alieleza kuwa wananchi wanawajibu wa kulinda mali za Shirika la Reli na ikiwa wananchi hawatashiriki ipasavyo italeta madhara makubwa katika ujenzi wa mradi wa SGR.

“Uhalifu si wizi pekee, hata kukatiza maeneo yaliyokatazwa, kumnyanyasa mtu kijinsia, kutoa rushwa au kumjeruhi mtu hayo yote ni mambo ya kiuhalifu na hatutayafumbia macho” aliongezea ACP Mapala.

Aidha, Diwani kutoka Kata ya Mabama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maendeleo katika kata hiyo ya Mabama Bi. Rehema Bushiri ameeleza kuwa elimu itaendelea kutolewa juu ya maswala ya kulinda miundombinu ya reli katika kila mikutano ya vijiji.

“Mikutano itaimarisha hali ya ulinzi na usalama kwani wananchi wanahitaji uelewa wakutosha na kujua kwamba huu mradi wa SGR unaopita katika maeneo yetu ni tunu kwetu na utaleta manufaa makubwa katika maeneo mbalimbali” alisema Diwani wa Kata ya Mabama Bi. Rehema Bushiri.

Naye Mwanasheria kutoka TRC Bi. Jane Kassanda ameelezea makosa ambayo yatapelekea wahalifu kupata adhabu kali ikiwemo kupeleka wanyama kwenye miundombinu ya reli , kurusha jiwe kwenye kioo cha treni, kutoboa njia sehemu pasipokua na njia, kuharibu miundombinu, kung’oa mataluma ambapo adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 na kuendelea pia kosa la uvamizi wa maeneo ya reli ambapo adhabu yake ni kifungo cha miaka miwili mpaka mitano au faini ya milioni tano mpaka kumi.

Maeneo ambayo timu kutoka TRC imefanya zoezi la uelewa kwa jamii ni pamoja na kijiji cha Izimbili, Ulamba, Tumbi, Ilolanguru, Mpenge na Isila vilivyomo katika wilaya ya Uyui - Tabora na kijiji cha Tumaini , Ulimakafu, Mabama, Ussoke, Usongelani, Sipungu, Usisya, Utemini, Ndono, Itundu, Mpigwa na Ullasa B vilivyomo katika wilaya ya Urambo mkoani Tabora.

Wajibu wa kulinda miundombinu ya reli ni wa kila mwananchi ili kuweza kudhibiti uhalifu unaoweza kujitokeza na kusababisha utekelezaji wa mradi wa SGR kutokamilika kwa wakati au kuleta athari za kiundeshaji pindi utapokamilika pia kusababisha ajali endapo kutatokea uharibifu katika njia ya reli.