WANANCHI WAENDELEA KUPOKEA STAHIKI ZAO MRADI WA SGR

February
2025
Shirika la reli Tanzania - TRC linafanya zoezi la ulipaji wa fidia katika kipande cha tano cha ujenzi wa mradi wa SGR kutoka Isaka hadi Mwanza kwa wananchi ambao makaburi ya ndugu na jamaa yalitwaliwa ili kupisha ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Reli ya kisasa - SGR hivi karibuni.
Zoezi hilo la hivi karibuni Februari 2025, limefanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kata ya Puni Wilaya ya Shinyanga, Kata ya Bungulwa Wilaya ya Kwimba, Kata ya Isemela Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga na Kata ya Sigili Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.TRC imelenga kulipa stahiki zote kwa wananchi wote ambao taarifa zao zilichukuliwa katika zoezi la uthamini wa maeneo hayo na kuhakikisha malipo ya fidia kwa wananchi husika yanafanyika.
Afisa Mazingira -TRC Bi. Nelly Mleleu, alisema kuwa TRC imeanza zoezi la kulipa fidia kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora, Shinyanga, Simiyu na Mwanza ambao walilazimika kuacha maeneo ambayo mkandarasi amehitaji katika kufanikisha Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) aidha wananchi wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano kwenye zoezi hilo ili liwe na ufanisi.
" Tunashukuru Uongozi wa vijiji, vitongoji, wananchi kwa kutupa ushirikiano mzuri na kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa urahisi, pia Uongozi wa TRC kwa kusimamia ujenzi wa mradi kwa kufuata usalama wa Mazingira pamoja na wananchi" alisema Bi. Nelly Mleleu Afisa Mazingira TRC
Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Puni Bw. Jackson Malia, alieleza kuwa Mradi wa SGR una manufaa makubwa , utawezesha wananchi kusafirisha mazao kwa urahisi kutoka Kijiji cha Puni kwenda mikoa mwingine ambapo itachagiza ukuaji na ueneaji wa biashara kwa haraka kwa wanakijiji, bidhaa na nafaka zitasafirishwa kwa urahisi na muda mfupi lakini ajira itaongezeka kwa wananchi.
" Timu kutoka TRC inahakikisha kila mwananchi anapewa haki yake kwa kulipwa hasa wale ambao walilazimika kuachia maeneo yao ili kupisha Ujenzi wa SGR, mradi huu unamanufaa katika kijiji chetu na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla" alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Puni Bw. Jackson Malia.
Katika hatua nyingine , mkazi wa Kijiji cha Puni Bw. Gilbert Mahudi ameishukuru Serikali kwa kuwapatia wananchi fidia na kusema kuwa wanakijiji wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutunza miundombinu ya reli kwani Mradi ni wa wanakijiji wote, hivyo ni jukumu letu kuutunza.
" Pesa niliyopitapa si yangu bali nitaitumia katika kuhakikisha najengea kaburi kama familia ilivyoelekeza, tunashukuru Uongozi kwa kutulipa wananchi fidia" ameeleza Bw. Gilbert Mahudi Mkazi wa Kijiji cha Puni
Zoezi hii ni endelevu katika Mikoa ambayo maeneo ya makaburi na mengineyo yalitwaliwa ilikupisha ujenzi wa SGR, Serikali chini ya usimamizi wa TRC itahakikisha na kuzingatia kila mwananchi anapatiwa stahiki ya eneo lake, pia kitendo cha wananchi kuachia maeneo hayo ni dhahiri kwamba wanaunga jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu katika kukuza na kuleta maendeleo kwa manufaa mapana ya taifa kwa ujumla.