WANANCHI WA KIGOMA WAHAMASISHWA KUUPOKEA MRADI UJENZI WA SGR

March
2025
Shirika la Reli Tanzania linaendelea na Kampeni ya Uelimishaji na Uhamasishaji jamii katika vijiji vitakavo pitiwa na mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha Uvinza - Malagarasi - Musongati Machi, 2025.
Kampeni hiyo ya Uelimishaji na Uhamasishaji inalenga kuelimisha na kuwajengea wananchi watakao pitiwa na mradi kufahamu na kuzingitia maswala mbalimbali yatakayojitokeza wakati wa ujenzi
Miongoni mwa masuala yanayozungumzwa katika kampeni hiyo, ni masuala ya Ulinzi na Usalama wa Mali za Mkandarasi na Mali za TRC , Utaratibu wa Kupokea na Kusajili maoni, Utunzaji Mazingira na namna ya utwaaji ardhi.
Akiongea wakati wa kikao kazi kati ya TRC na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Bwana Sangu Deogratius amesema kuwa kupitia Shirika la Reli Tanzania nchi imeweza kuwa mfano wa kuigwa na nchini zingine barani Afrika kwa kuboresha sekta ya usafiri wa reli hiyvo kuitaka TRC ifanye kazi kwa weledi na haraka kukamilisha ujenzi wa reli ya SGR ambayo itaiunganisha Tanzania na Burundi.
" Niishukuru TRC kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ambayo imeonesha katika ujenzi wa SGR wa vipande vya awali, naamini ujenzi huu wa SGR mpaka Burundi utakamilika kwa wakati ili kuleta tija iliyokusudiwa na nchi hizi mbili za kukuza biashara na ushirikiano" amesema Bwana Sangu.
Aidha, Bwana Sangu ameipongeza TRC kuratibu kampeni hii ya uelewa kwani itasaidia kurahisisha kazi ya ujenzi kwa kuleta hamasa, kujenga Uaminifu na Ushirikiano baina ya wananchi , TRC pamoja na Mkandarasi.
Meneja Mradi ujenzi wa SGR kipande cha 7 & 8 ( Uvinza - Musongati) kutoka TRC Mhandisi Manoni Bundu ameeleza kuwa TRC imejipanga kuandaa na kufanya Kampeni mbalimbali za uelewa kwa jamii ili kuhakikisha inondoa migogoro na kuiwezesha jamii ya watanzania kufaidika na ujenzi wa SGR .
" Kampeni hii sio ya mwisho ,TRC itafanya kampeni kama hizi nyingi sana wakati wa ujenzi wa SGR ,kila kampeni itabeba dhima tofauti ili kuhakikisha jamii inauelewa na kufahamu maswala mbalimbali na kuondoa migogoro itakayokwamisha ujenzi " Amesema Mhandisi Manoni.
Kampeni ya kujenga Uelewa na Uhamasishaji jamii inaendelea Mkoa wa Kigoma katika Wilaya za Uvinza na Kasulu katika vijiji 25 ambavyo vitapitiwa na mradi wa Ujenzi wa SGR kipande cha 7 & 8 Uvinza - Musongati.