Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI MKOANI SHINYANGA, SIMIYU, MWANZA WAIPA HEKO SERIKALI


news title here
07
February
2025

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora, Shinyanga, Simiyu na Mwanza, waliotwaliwa ardhi ili kupisha Mradi wa Ujenzi wa reli itumiayo nishati ya umeme - SGR Kipande cha tano kutoka Isaka hadi Mwanza hivi karibuni.

Wananchi wa Kata za Kanyelele, Ukirigulu, Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, Kata ya Badi, Malampaka, Mataba, Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, pamoja na Kata ya Usulu Wilaya ya Shinyanga na Kata ya Bukene Wilaya ya Shinyanga vijijini Mkoani Shinyanga wamepatiwa stahiki zao na timu kutoka TRC ambapo wametoa pongezi kwa TRC kwa niaba ya Serikali kwa kuhakikisha wananchi husika wanapokea hundi zao za malipo.

Aidha Mhasibu kutoka TRC Bw. Edgar Alibaliho emeeleza kuwa, TRC inatambua umuhimu wa wananchi kuachia maeneo yao kuipa nafasi serikali kufanya shughuli za maendeleo hususani mradi wa SGR ambao ni chachu ya maendeleo nchini Tanzania kwa ujumla pamoja na nchi jirani kama Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo na Burundi.

" Mradi wa SGR utachagiza urahisi wa usafirishaji wa abiria aidha mizigo itasafirishwa kwa wingi na kwa wakati mmoja na kuchochea Maendeleo halikadharika kukua kwa biashara" aliongezea Bw. Alibaliho

Katika hatua nyingine, Bw. Emmanuel Ernest Afisa Mtendaji Kijiji cha Nyashimbas Kata ya Badi Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, amesema wananchi wamefurahi kulipwa fidia ya maeneo yao kupisha Ujenzi wa mradi wa SGR. Aidha alisema kuwa Mradi huo utarahisisha shughuli za usafirishaji na pia kutoa fursa kwa wafanyabiashara katika kukuza biashara na kuongeza kipato kwa Kaya zao.

" Mradi umepita katika maeneo yetu, natoa wito kwa wananchi kua tayari kuulinda na kuutunza kwa kuuthamini kwani utasaidia jamii nzima na kuongeza pato la taifa " amekazia Bw. Emmanuel Ernest Mtendaji wa Kijiji cha Nyashimbas Kata ya Badi

Wakati huo huo Mkazi wa Kijiji cha Bukene Kata ya Bukene Wilaya ya Shinyanga Bw. Elias Mhoja, ameeleza kuwa jamii za wakulima na wafugaji Shinyanga, zitanufaika na uwepo wa mradi wa SGR pindi utakapokamilika katika kusafirisha mizigo lakini pia ameshukuru serikali kutambua umuhimu wa wananchi kupata haki zao kupitia zoezi la ulipaji fidia.

"Kulingana na ushindani wa soko itatulazimu kuwahi soko kwa wakati, hivyo SGR ni suluhisho kamili katika kusafirisha mizigo kwa muda mfupi" ameeleza Bw. Elias Mhoja Mkazi wa Kijiji cha Bukene Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga.

Timu maalumu kutoka TRC inaendelea na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wa Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga waliotwaliwa ardhi kupisha Ujenzi wa reli ya SGR, ili kuchagiza maendeleo katika kukuza pato la taifa kiuchumi kuanzia mtu mmoja, familia, jamii na Taifa kwa ujumla.