Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI JIJINI MWANZA WASHUKURU UJIO WA MRADI WA SGR


news title here
02
March
2021

Wananchi wa kijiji cha Nyamatala kata ya Ukiliguru wilaya ya Misungwi jijini Mwanza wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujio wa Mradi wa Reli ya Kisasa – SGR jijini humo kufuatia hatua za awali za maandalizi kwa ajili ya mradi huo kuanza, hivi karibuni Machi 2021.

Wananchi wamezungumza hayo walipokuwa wakipokea hundi kwa ajili ya malipo ya fidia ya maeneo yao yaliyotwaliwa kwa ajili ya kituo cha kupakua na kupakia mizigo kwa ajili ya treni za reli ya kisasa kitakachojengwa sambamba na bandari kavu katika eneo la Fela jijini humo.

Wananchi zaidi ya 70 wamekabidhiwa hundi zao katika zoezi lililofanyika kwa siku mbili katika kijiji cha Nyamatala ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 2 zimetumika kwa ajili ya malipo hayo.

Diwani wa Kata ya Ukiliguru Bwana Mathew Makoye ametoa Shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi ya kulipa fidia kwa wananchi wa kata hiyo na kuongeza kuwa wananchi wamepokea stahiki zao na wameridhika.

Bwana Mathew alisisitiza kuwa “Mimi na wananchi wangu tumeupokea kwa mikono miwili, kwa sababu mradi huu utakapokamilika utasaidia katika usafiri muda utakaotumika utakuwa ni Saa 6 hadi 7 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwahiyo utakuwa na tija kwa wananchi”

Naye mmoja wa wananchi waliopatiwa fidia ili kupisha mradi huo Bwana Lucas Justine ameeleza hisia zake mara baada ya kupatiwa stahiki yake na kusema kuwa “Tumekuja kuchukua hundi kwa ajili ya malipo ya fidia ya maeneo yetu yaliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa SGR, tunapongeza ujio wa reli hii na tutapata fursa za ajira na biashara kupitia mradi huu”

Utekelezaji wa Mradi wa SGR kipande cha 5 Mwanza – Isaka unatarajiwa kuleta fursa za ajira na biashara kwa wananchi hususani wanaoishi kando ya maeneo ambayo mradi huo utakaohusisha ujenzi wa reli yenye urefu wa Kilometa 341, kituo cha Mizigo eneo la Fela na vituo vya reli takribani 7, sambamba na fursa hizo reli hii itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji mizigo kati ya Dar es Salaam na nchi za jirani ikiwemo Uganda na Sudani kusini.