Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WANANCHI IHUMWA WAISHUKURU SERIKALI NA TRC KWA KUWALIPA FIDIA ILI KUPISHA UJENZI WA SGR


news title here
28
July
2020

Shirika la Reli Tanzania laendelea na zoezi la ulipaji wa fidia kupisha ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha Morogoro - Makutupora, katika kata ya Ihumwa mkoani Dodoma hivi karibuni.

Katika awamu hii ya Ulipaji wa fidia kwa wakazi wa kata hiyo ambao maeneo yao yalitwaliwa na mradi, kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni moja kimetengwa na jumla ya watu 810 watalipwa wakati wa zoezi hilo litakalodumu kwa majuma mawili.

Hadi sasa jumla ya wakazi 231 wa kata ya Ihumwa wameshalipwa fedha zao ikiwa ni siku tatu tu tangu kuanza kwa zoezi hilo la ulipaji wa fidia.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Ihumwa waliolipwa stahiki zao wameelezea furaha yao na shukurani kwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Jemedali Dokta John Pombe Magufuli na shirika la Reli Tanzania kwa kuhakikisha wanapata fidia hizo.

Mmoja wa wakazi hao Bw. Dickson Chiwanga,amesema “naipongeza sana serikali kwa hatua hii kwani kitu wanachofanya ni cha kutuletea maendeleo na tutakitumia wote kwa pamoja”

Kuhusu matumizi ya fedha hizo, wananchi hao wameeleza kuwa fedha hizo zitawasaidia katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo biashara,kilimo,ufugaji na kuanzisha makazi mapya.

“hii pesa itanisaidia mambo mengi, kibiashara lakini pia naweza nikajenga hivyo naweza kutoka hatua moja kwenda nyingine” alisema Bw. Henry Shedrack, ambae ni mmoja kati ya wakazi wa kata ya Ihumwa waliolipwa fidia

Aidha wananchi hao wamewataka wenzao ambao bado hawajalipwa fidia kupuuzia uzushi unaosambazwa na wachache kuwa fedha hizo hazitalipwa na kusisitiza kuwa ni uongo na kwamba wote watalipwa haki zao kama ilivyokuwa kwao.

Zoezi hilo la ulipaji wa fidia linaendelea wakati ambapo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Morogoro - Makutupora, umefikia 38%