Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAKULIMA KUFAIDIKA KUPITIA MKAKATI MPYA WA UPATIKANAJI MIZIGO


news title here
02
October
2024

Shirika la Reli Tanzania kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limezindua Mkakati wa Upatikanaji Mizigo wa Kuimarisha Biashara ya Usafirishaji Nchini kwenye hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya stesheni ya Reli ya Kati (MGR) Kilosa mkoani Morogoro Oktoba 01, 2024.

Lengo kuu la Mkakati wa upatikanaji wa mizigo wa Kuimarisha Biashara ya Usafirishaji nchini ni kuwezesha sekta ya Uchukuzi kupitia ujenzi wa reli na uboreshaji wa miundombinu ili kuchochea maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla kupitia kilimo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema Serikali kupitia TRC imelenga kurahisisha uzalishaji katika kilimo kwa kuwezesha usafirishaji wa malighafi ya kilimo, wakulima, wafanyakazi na vilevile kukuza biashara za nje na utafutaji masoko.

"Mpango wa Serikali ni wa kimkakati na uhakika kwani unatarajia kuleta matokeo chanya ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya nchi na jamii kwa ujumla" Amesema Kihenzile.

Aidha, Mhe. Naibu Waziri ameongeza kuwa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu Miundombinu ya reli imechochea kwa kiasi kikubwa katika kukuza ajira, kuongeza pato la nchi kupitia kodi na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia Biashara na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi na biashara kupitia fursa ya kijografia iliyo nayo.

Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amesema kuwa uzalishaji, utunzwaji na Usafirishaji wa mazao yenye kuharibika haraka (Horticulture) unahitaji utaalamu na miundombinu madhubuti kuyafanya yasiharibike ili kuweza kutunza ubora wake na kuwafikia walengwa yakiwa katika hali nzuri.

Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa Ushirikiano baina ya TRC na WFP umefungua fursa za biashara kupitia bandari ya Dar es Salaam na nchi zisizo na bandari.

"Ushirikiano wa TRC na WFP ulianza zamani, lakini mwaka 2023 taasisi hizi mbili ziliingia makubaliano rasmi ya kunyanyua fursa za biashara na WFP ilikabidhi mabehewa 40 ya mizigo kwa TRC ili kusafirisha mizigo, uhusiano huu bado unaendelea na leo tuko hapa tunashuhudia namna gani mabehewa ya Makasha ya ubaridi yatasaidia wakulima kuuza bidhaa zao" Amesema Ndugu Kadogosa.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani Kanda ya Tanzania Bwana Ronald Tran Ba Huy ameeleza kuwa lengo la WFP ni kuunganisha wakulima kutoka maeneo ya uzalishaji wa chakula mikoa ya Morogoro na Dodoma na wanunuzi na wenye viwanda nchini na nje ya nchi ili kuinua uchumi na nchi na jamii.

Kupitia uzinduzi wa Mkakati wa Upatikanaji Mizigo wa Kuimarisha Biashara Usafirishaji nchini wakulima watapata fursa ya uhakika wa masoko ya ndani na nje ya nchi na kuboresha maisha yao ya kila siku.