Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

VIONGOZI WA JUU WA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO WAKIONGOZWA NA DKT. ABBAS WATEMBELEA MRADI WA SGR


news title here
26
September
2020

Viongozi wa juu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo Dkt. Hassan Abbas wametembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kipande cha Morogoro – Makutupora kuona maendeleo ya mradi huo, Septemba 25, 2020.
Viongozi hao wanatarajiwa kuendelea na ziara hiyo ambapo watatembelea pia kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ili kutimiza ziara hiyo ya kikazi ya siku mbili lengo likiwa ni kushiriki kikamilifu katika kuutangaza mradi huo wa SGR kwa umma wa watanzania ili uweze kufahamu faida pamoja na fursa lukuki zinazopatikana katika mradi huo.
Ziara hiyo imeanzia jijini Dodoma katika kambi ya mradi Ihumwa ambapo viongozi hao walipata fursa ya kusikiliza mada iliyowasilishwa na Meneja Mradi wa SGR Morogoro – Makutupora Mhandisi Titto Mateshi kuhusu maendeleo ya mradi kwa kipande hicho ambao umefika zaidi ya 42%, sambamba na hilo viongozi walipata nafasi ya kuuliza maswali kadhaa kwa lengo la kuongeza uelewa.
Katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbas ambaye ndiye kiongozi wa ziara hiyo alieleza kuwa uwekezaji huanza katika vitu na baadae hupelekea maendeleo ya watu kwa maana hiyo Wizara ikiwa na jukumu la kutoa habari inayo jukumu la kuhakikisha Miradi ya aina hii inafahamika na inaleta manufaa
“Wizara ya Habari ni wizara muhimu sana katika nchi yetu hususani katika mradi huu kwa sababu ndiyo yenye dhamana ya kutoa habari na imekuwa ikiuntangaza sana mradi huu, mradi wetu ni miongoni mwa miradi mikubwa Barani Afrika” alisema Dkt. Abbas
Naye Bi. Leah Kihimbi Ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesma kuwa amefurahishwa na mradi huo kwa maendeleo yake lakini pia ameahidi kwa niaba ya Wizara kuwa watajipanga kuhakikisha wanautangaza mradi huo wa kimkakati.
“Mradi huu unafanya vizuri sana, tumeshuhudia watanzania wanafanya kazi kwa kweli ni mradi mzuri sana, sisi kama Wizara ya Habari tunajivunia sana mradi huu jukumu letu ni kuutangaza ili wananchi wauelewe na waahamu faida zake” alisema Bi. Leah