Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

VIONGOZI MBALIMBALI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WASIFU MRADI WA SGR


news title here
26
June
2021

Viongozi mbalimbali kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki waisifu nchi ya Tanzania pamoja na Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR walipotembelea mradi kuanzia stesheni ya Dar es Salaam hadi Pugu, Juni 25, 2021.

Viongozi hao ni pamoja na wakurugenzi mbalimbali, wawakilishi wa makatibu wakuu wa Jumuiya ya Afika Mashariki kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na Balozi wa Sudani Kusini Tanzania ambapo wamepata fursa ya kuona maendeleo ya mradi wa SGR na ufanisi mkubwa uliotumika katika ujenzi huo.

Pia viongozi hao walitembelea katika kituo cha kwanza chenye mitambo ya kupoozea umeme kilichopo katika eneo la Pugu na kupata maelezo juu ya mitambo hiyo itakavyoweza kufanya kazi kudhibiti umeme mkubwa na kupeleka kiwango cha umeme utakaohitajika kwenye uendeshaji wa treni.

Mkurugenzi wa huduma ya Usambazaji Hewa kutoka katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Sudani Kusini Bw. Stephen Rombe amefurahishwa sana kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa na kusema kuwa mradi huo utafika mbali hadi kufikia katika mipaka ya nchi jirani kwa ajili ya kukuza uchumi katika nchi za Afrika Mashariki na kati.

"Tanzania imefanya kitu kikubwa ambacho jumuiya za nchi nyingine za Afika zinatakiwa kufanya miradi mikubwa kama huu" alisema Bw. Rombe.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Ujenzi TRC Mhandisi Faustine Kataraia amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu sana kwa TRC kwa kupata ugeni kutoka nchi za Afrika kwa kutambua kitu kinachofanywa na TRC katika kuimarisha miundombinu ya reli.

Mhandisi Kataraia ameeleza kuwa miundombinu ya reli itaimarisha uchumi wa nchi ya Tanzania pamoja na nchi jirani kwa usafirishaji wa mizigo na pia itasaidia kulinda barabara kwa kupitisha mizigo yenye uzito mkubwa kwa njia ya treni.