UJENZI WA SGR UVINZA - MALAGARASI - MUSONGATI KUIBUA FURSA ZA AJIRA NA BIASHARA KIGOMA

March
2025
Shirika la Reli Tanzania (TRC), linaendelea kuhamasisha vijana na wananchi kujiunga na vyuo vya ufundi stadi pamoja na taasisi zinazotoa mafunzo ya ujuzi kuwawezesha kupata ajira katika mradi wa SGR kipande cha 7 & 8.
Wiki hii Kampeni ya Uelewa na Uhamasishaji wananchi imefanyika katika vijiji 25 vya Wilaya ya Uvinza, Kasulu na Buhigwe Mkoa wa Kigoma, ambapo imelenga kuwahamasisha wananchi kuhusu faida na mafanikio ya ujenzi wa SGR ikiwemo ongezeko la ajira, kukua kwa biashara ndogo ndogo na kubwa, muingiliano wa watu kutoka jamii mbalimbali na kukua kwa sekta nyingine kama kilimo na utalii.
Meneja Mradi Ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha 7 & 8 kutoka TRC Mhandisi Manoni Bundu, amewaasa vijana kuchangamkia fursa ambazo zitatokana na ujenzi wa reli ya SGR zikiwemo nafasi za kazi za ofisini , madereva, mafundi, wapishi, wafanya usafi, biashara za vyakula na nyumba za kulala wageni.
" Kampeni hii imelenga kuelimisha wananchi kuupokea, kuumiliki na kuutambua mradi na fursa zilizopo kwasababu miundombinu inayojengwa ni ya Watanzania wote na walipa kodi, kwa hiyo ni jambo la muhimu TRC kufanya Kampeni ya uelimishaji kwa wananchi kabla mkandarasi hajaanza ujenzi" amesema Mhandisi Bundu
Aidha, Mhandisi Bundu, amewasihi wananchi kuilinda na kuisimamia vyema miundombinu ya reli kabla na baada ya ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati na kuepusha migogoro.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni, Wilaya ya uvinza- Kigoma, Bwana Saidi Ramadhani, amesema viongozi wa vijiji wanapswa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha miradi iliyoanzishwa inakamilika kwa wakati.
"'Eneo letu awali lilionekana la kawaida hakuna mtu alilitaka lakini kwa sasa tunapokea watu mbalimbali wanafanya uwekezaji mkubwa, kwa hili nataka kusema kuupokea mradi wa SGR kwa kweli nifuraha sana na kama mwenyekiti nitahakikisha nasimamia wananchi wangu ili kufanikisha ujenzi huu" alisema Bwana Ramadhani.
Wakati huo huo, Bi.Agnetta Blushi Mkazi wa Kasulu - Kigoma amefurahishwa na ujio wa ujenzi wa Reli ya SGR nakuwasihi kinamama wajasiriamali kujiunga na vikundi vya maendeleo ya kinamama ili waweze kunufaika kupitia mafunzo na mikopo ya vikundi itakayo boresha biashara zao na kuweza kunufaika na mradi wa SGR.
Shirika la Reli Tanzania linaendelea Kuelimisha na Kuhamasisha wananchi kuhusu Ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha 7 & 8 cha Uvinza Malagarasi - Musongati ambapo utekelezaji wa ujenzi Umeanza katika hatua za awali .