Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​UGANDA KUNUFAIKA NA UZOEFU WA TANZANIA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA SGR


news title here
06
November
2026

Shirika la Reli Tanzania (TRC), Novemba 5, 2026 limepokea ugeni wa Kamati ya Bajeti ya Bunge kutoka nchini Uganda katika Stesheni ya John Pombe Magufuli ya SGR jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, ameupokea ugeni huo, ambapo katika mazungumzo na ugeni huo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda kupitia sekta ya reli ni muhimu katika kuimarisha biashara, usafirishaji na muunganiko wa kiuchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu.

Aidha Mhandisi Shiwa, amesema ziara hiyo ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli, hususan Reli ya Kisasa (SGR).

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Uganda Mhe. Tom Aliti, ameishukuru TRC kwa mapokezi mazuri na ukarimu, akieleza kuwa wamejifunza mambo muhimu yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa mradi wa SGR nchini Uganda. Amebainisha umuhimu wa kushirikisha wadau katika usanifu wa miradi, kuzingatia matumizi ya rasilimali za ndani na kuweka vipaumbele vya kifedha ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Mastula Namatovu, ameipongeza Tanzania kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya reli, akieleza kuwa uzoefu walioupata utawasaidia katika kufanya maamuzi ya kibajeti na kuweka mikakati ya kuendeleza miradi ya kimkakati nchini Uganda.

Ziara hiyo inadhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kubadilishana uzoefu katika kukuza sekta ya reli, kufungua masoko na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo baina ya nchi za Afrika Mashariki