TRENI YA MCHONGOKO YAANZA RASMI SAFARI DAR ES SALAAM - DODOMA
November
2024
Shirika la reli Tanzania -TRC limeanzisha rasmi usafirishaji wa abiria kwa kutumia treni ya Electric Multiple Unit - EMU maarufu treni ya mchongoko kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma tarehe Novemba 1, 2024.
Safari ya kwanza ya treni hiyo iliyoanzia Dar es Salaam saa mbili asubuhi na kufika Dodoma majira ya saa tano asubuhi nakupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuipokea treni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alieleza kuwa treni za haraka na za kawaida zinazotumia nishati ya umeme zimeendelea kufanya vizuri katika kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria tangu kuzinduliwa, ongezeko la treni za EMU (mchongoko) zitaendelea kuleta tija na thamani ya usafirishaji kwa kutumia reli yenye kiwango cha kimataifa.
“Treni ya EMU ina uwezo wa kubeba jumla ya abiria 589 lakini waliosafiri leo na treni hii abiria 320 ambao watakua mashuhuda wa kwanza kusafiri na EMU kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma" alisema Mhe. Rosemary.
Mhe. Rosemary amepongeza jitihada zinazofanywa na serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza miundombinu ya reli pamoja na kutengeneza mazingira rafiki kwa TRC ili kuhakikisha inajengwa miundombinu imara yenye kiwango cha juu, pia ameiongeza TRC kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa abiria.
"Naipongeza TRC wameweka safari za treni ya reli ya kisasa siku nzima kuanzia alfajiri hadi jioni na kuwezesha wananchi wa Dodoma na watu kutoka mikoa mbalimbali kusafiri kwa muda wanaotaka" alieleza Mhe. Rosemary.
Mhe. Rosemary alizungumza kuwa zaidi ya watu 3000 wanaingia mkoani Dodoma na zaidi ya watu 3000 wanaondoka mkoani humo kupitia treni za mwendokasi.
"Sisi kwa mkoa wa Dodoma tumeendelea kuona mabadiliko makubwa ya wananchi wakifurahia ongezeko la mapato kupitia treni za SGR wakiwemo bodaboda, bajaji, dereva taxi, wauza vyakula pamoja na hoteli” alisema Mhe. Rosemary.
Awali kabla ya treni hiyo kuanza safari katika stesheni ya SGR ya Magufuli, Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kadogosa alisema kuwa Shirika limeongeza safari zingine kwa kutumia treni hiyo ya EMU (mchongoko) ambayo safari zake zitakua na utofauti kiasi ukilinganisha na safari za treni nyingine za SGR.
“Treni ya mchongoko itakua na utauti kidogo kwakuwa hii haitasimama Kilosa, itatoka Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma” alisema Ndugu Kadogosa.
Pia Ndugu Kadogosa alieleza kuwa kwa sasa kutakua na treni nne za kwenda na treni nne za kurudi ambapo safari za treni ya Morogoro zitabaki kama zilivyo.
“Kwa siku TRC inasafirisha abiria zaidi ya elf tisa na muitikio wa watu ni mkubwa sana” aliongezea Ndugu Kadogosa.
TRC inaendelea kutoa huduma za usafirishaji abiria kwa kutumia reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR na kuendelea kuweka mazingira imara ya mifumo ya ukataji wa tiketi kwa kutumia njia ya mtandao ambao inatoa urahisi kwa abiria.