Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRENI YA KWANZA YA MIZIGO YA MAJARIBIO YAWASILI JIJINI ARUSHA BAADA YA ZAIDI YA MIAKA 30


news title here
13
August
2020

Treni kwanza ya mizigo ya majaribio yawasili katika Stesheni ya Arusha baada ya zaidi ya miaka 30 ikitokea Tanga na kupokekewa na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika Stesheni Arusha Agosti 13, 2020.

Treni hiyo imewasili jijini Arusha ikiwa na shehena ya tani 400 za Saruji, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini Mhe. Kenani Kihongsi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Kimanta aliungana na wananchi wa Arusha kuipokea treni hiyo. Katika tukio hilo la kihistoria Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Jerry Muro aliungana na watumishi kutoka Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kupanda treni hiyo kutoka Stesheni ya Usa River hadi stesheni ya Arusha.

Kurejeshwa kwa safari za treni kwa reli ya Kaskazini ni moja kati ya utekelezaji mkubwa wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kurejesha huduma hiyo ambapo Julai 2019 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua rasmi usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam na Moshi ambapo huduma zinaendelea na hivi karibuni huduma za usafiri wa treni Dar es Salaam, Tanga na Arusha zitazinduliwa rasmi baada ya majaribio ya njia kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Tumekuja kuwaambia kwamba kazi ya miaka mitano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi leo inakamilika katika mkoa wetu wa Arusha” alisema Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Jerry Muro

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini aliongeza kuwa ni zaidi ya miaka 30 reli hiyo imeacha kufanya kazi na baadhi ya wananchi wamezaliwa hawajawahi kuiona treni lakini kwa kipindi cha miaka mitano ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli treni imeweza kufika Arusha na wananchi wanaanza kunufaika na fursa zilizoletwa na treni hiyo.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kuipokea treni hiyo wameeleza maoni yao juu ya kurejea kwa huduma hizo ambapo wameonesha kufurahishwa na maamuzi hayo na kuonesha utayari wa kuchangamkia fursa zitokazokuwepo ikiwemo biashara na ajira ambazo zimeanza kuonekana mara baada ya treni ya shehena ya saruji kuwasili jijini hapo ambapo vijana wamejipatia kibarua cha kupakua mizigo kutoka kwenye treni.

“Treni hii tumeipokea kwa mikono miwili, tumefurahi na tunaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli aweze kufanya yale yanayomgusa kila mtu ili maendeleo ya leo na kesho, kwa sababu Saruji tunayonunua leo 15,000 itapungua bei kutokana na usafiri huu nafuu” alisema James Peter mkazi wa jiji la Arusha.

Sambamba na kuwasili kwa treni ya majaribio iliyobeba Tani 800 za Saruji, Shirika la Reli linaendelea na kutoa elimu ya uelewa katika Shule, maeneo ya mikusanyiko ikiwemo Vituo vya Mabasi, Pikipiki na mikutano ya wananchi kuhamasisha wananchi kutunza miundombinu ya reli na kuzingatia usalama katika maeneo ya reli ili kuepusha ajali.