Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRENI YA KWANZA YA ABIRIA YAWASILI JIJINI ARUSHA BAADA YA ZAIDI YA MIAKA 30


news title here
25
August
2020

Treni ya kwanza ya abiria ya majaribio yawasili jijini Arusha ikitokea Dar es Salaam na Moshi na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Hassan kimanta, viongozi wa Chama na Serikali mkoani humo pamoja na maelfu ya wananchi wa jiji la Arusha waliojitokeza katika stesheni ya Arusha Agosti 24, 2020.

Safari ya treni kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro iliruhusiwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira ambaye alipeperusha bendera kuashiria kuanza rasmi kwa safari hiyo ya majaribio kutoka Moshi kuelekea jijini Arusha.

Katika safari hiyo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro aliongozana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapionduzi Ndugu Humphrey Polepole, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro na maafisa wa Shirika la Reli wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa

Aidha katika safari hiyo treni iliweza kusimama katika vituo kadhaa ikiwemo Masama Rundugai pamoja na Usa River ambapo maelfu ya wananchi walijitokeza kuilaki treni hiyo ya majaribio na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipata fursa ya kupiga simu na kuwasalimia wananchi wa Usa River waliojitokea kuilaki treni hiyo.

Mhe. Rais kupitia mazungumzo ya simu amelipongeza Shirika la Reli kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kurejesha huduma ya usafiri wa treni katika njia ya kaskazini iliyosimama kwa zaidi ya miaka 30 na kuathiri shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii

“Nawapongeza sana kwa kuipokea treni hiyo, nafahamu kwamba wakazi wa Arusha na maeneo mbalimbali mkiwemo wa Usa River mliteseka kwa miaka mingi kwa zaidi ya miaka 30, nataka niwahakikishie kwamba treni ya mizigo na abiria zitaanza kufanya kazi na Mungu awasaidie mchape kazi, mfanye biashara tuijenge Arusha na Tanzania, nawapongeza pia wafanyakazi wa TRC kwa kuchapa kazi” alisema Rais Magufuli.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Ndugu Humphrey Polepole amesema kuwa lengo la kujumuika katika safari hiyo ni kufanya ukaguzi na majaribio ya njia hiyo ili ianze rasmi kufanya kazi baada ya majaribio ya treni ya mizigo kufanikiwa hivi karibuni.

“Siku chache zilizopita tulipitisha treni ya majaribio iliyobeba mizigo, tumekuja kukagua kama njia hii iko tayari kubeba abiria, tumetoka Moshi tumesimama kituo kwa kituo kujiridhisha kama miundombinu ipo na kuna watu katika kila kituo, tumekuta madaraja makubwa zaidi ya 10 yamejengwa” alisema Polepole

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kwani lilifanyika mwaka 2019 kutoka Dar es Salaam hadi Moshi na huduma kuanza baadaye, hivyo tukio hilo ni muendelezo wa kuhakikisha safari za treni kuelekea Arusha zinarejea kwani zoezi la majaribio ni la kisheria ili huduma ziweze kuanza rasmi.

“Mwaka jana tarehe 09 Desemba 2019 tulishuhudia tukio kama hili tulifanya majaribio ya treni kutoka Dar es Salaam hadi Kilimanjaro, lakini pia tunaushukuru uongozi wa Mkoa wa Arusha kwakuwa tukio hili lilianza kuhamasisha wananchi kutunza miundombinu ya reli kwa kweli Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro mmetusaidia sana pamoja na wakuu wa wilaya” alisema Kadogosa

Mkurugenzi Mkuu amewasihi wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya reli kwa kuwa reli hiyo ni ya watanzania wote, sambamba na hilo ameeleza umuhimu wa reli hiyo ikiwemo kupunguza gharama za bidhaa, kutunza barabara, kupunguza ajali lakini pia reli hiyo itasaidia wakati wa ujenzi wa reli ya kisasa -SGR kutoka Tanga - Moshi - Arusha hadi Musoma kwa kusafirisha mizigo na vifaa vya ujenzi wa reli mpya ya viwango vya kimataifa.