Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YA ZINDUA KAMPENI YA UELEWA KUHUSU KUANZA HUDUMA ZA UENDESHAJI TRENI ZA SGR DAR ES SALAAM- MOROGORO


news title here
12
June
2024

Shirika la Reli Tanzania lazindua kampeni ya uelewa kuhusu kuanza kwa huduma za safari za treni katika Reli ya kiwango cha Kimataifa - SGR kwenye hafla fupi iliofanyika stesheni ya SGR Dar es Salaam, Juni 12, 2024.

Kampeni inalengo la kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya huduma mpya za SGR pamoja na mambo muhimu yakuzingatia katika masuala ya ulinzi na usalama wa abiria na mali zao ambapo kaulimbiu ya kampeni ni "Twende Tukapande Treni Yetu, Tuitunze, Tuithamini"

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa katika utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha huduma za usafiri wa Treni zinaanza, Shirika la Reli Tanzania limeendelea kuchukua hatua kuhakikisha utekelezaji wa kuanza huduma za uendeshaji zinafanyika.

"Katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika linautaarifu umma kuanza kwa utoaji huduma za awali za usafiri wa treni za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro ifikapo Juni 14, 2024 " amesema Kadogosa.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa kuanza kwa safari za treni za abiria kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni baada ya Shirika la Reli Tanzania kujiridhisha na utayari wa Miundombinu, Vitendea kazi (vichwa na Mabehewa) na mifumo ya Ishara na Mawasiliano.

"Shirika limefanya majaribio kadhaa kwa lengo la kujifunza na kukamilisha matakwa ya kisheria kuhakikisha vitendea kazi, njia na mifumo ya mawasiliano vimekidhi ufanisi na ubora kwaajili ya usalama wa abiria" ameongeza Ndugu Kadogosa.

Sambamba na hilo Mkurugenzi Kadogosa amewasihi wananchi kutumia huduma za usafiri wa treni kwani kupitia usafiri huo abiria wataweza kupata huduma zote ndani ya treni ikiwemo chakula, maliwato, mazingira mazuri ya kufanya kazi wakiwa safarini, huduma za mtandao pamoja na burudani.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) Bwana Adam Mihayo amesema kuwa Benki ya Biashara Tanzania imeshirikiana bega kwa bega na Shirika la Reli Tanzania katika ujenzi wa mradi wa kimkakati wa SGR kuhakikisha mahitaji ya Watanzania yanatimia na kukuza uchumi wa nchi .

"Katika mradi huu wa kimkakati wa ujenzi wa SGR, TCB imeshirikiana na TRC katika maeneo ya kulipa wazabuni na ununuzi wa vichwa na mabehewa kutoka Ujerumani, hii imekuwa faraja Kwetu" amesema Bwana Mihayo

Mihayo aliongeza kuwa "Tumeingia pia makubaliano na TRC ya ukusanyaji wa malipo kupitia ukataji tiketi, mfumo mzima utasimamiwa na TCB na makusanyo ya pesa taslimu, pia yatasimamiwa na Benki yetu na kama TCB niwaahahidi Watanzania tutaendelea kutoa huduma bora kwa kushirikiana na TRC ili kutimiza matarajio ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania".

Afisa Biashara kutoka Shirika la Reli Tanzania Bi. Liliani Mselle amefafanua njia za ukataji tiketi za usafiri wa Treni za SGR kupitia njia ya mtandao na madirisha ya tiketi ndani ya stesheni za SGR. Shirika la Reli limeanisha aina na madaraja mbalimbali ya treni zitakazotumika katika usafirishaji wa awali ambapo kutakuwa na treni za kawaida ambazo zitasimama kila kituo kutoka Dar es Salaam – Morogoro na treni za mwendo wa haraka (express) ambazo zitatoka moja kwa moja bila kusimama kituo chochote kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Kadhalika upande wa treni za mchongoko (EMU) zitakuwa na madaraja yafuatayo, Daraja la Juu (High Class), Daraja la Uchumi (Economy Class), Daraja la Biashara (Business Class) na Daraja la Kifalme la Biashara (Royal Business Class).

Shughuli za treni za SGR kutoka Dar Es Salaam - Morogoro zinatarajia kuanza rasmi safari kutoka Dar Es Salaam - Morogoro Juni 14, 2024.