TRC YASISITIZA KILA MWANANCHI ANA WAJIBU WA KUILINDA MIUNDOMBINU YA RELI
December
2024
Kitengo cha Habari kwa kushirikiana na maafisa wa TRC kutoka vitengo vya Ulinzi na Usalama wa Reli, Ishara na Mawasiliano, Polisi Reli, Masuala ya Jamii wamehitimisha kampeni ya uelewa kwa wananchi juu ya ulinzi wa miundombinu ya reli na vitendea kazi vya uendeshaji Wilayani Ilala Mkoani Dar es Salaam. Zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano na viongozi wa Serikali kwenye maeneo yaliyo pembezoni mwa reli ya SGR na MGR Disemba 11, 2024.
Reli ya kati na SGR kwa Mkoa wa Dar es Salaam, imepita katika wilaya ya Ilala na zoezi hili kwa wilaya hiyo limefanyika Pugu Mnadani, Guluka Kwalala na Gogo la Mboto aidha elimu inaendelea kutolewa kupitia matangazo katika maeneo ya Mombasa & Ukonga, Banana, Airport, Kipawa, Vingunguti, Buguruni, Ilala, Kamata, Nkurumah (Gold Star) na maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Magomeni, Kariakoo, Fire, Jangwani, Kigogo,Tabata, kinyerezi, Ulongoni, Posta, Mnazi Mmoja, Kisutu na mengine jijini Dar es Salaam.
Afisa Polisi Jamii kutoka kikosi cha Reli ACP Venance Mapala, amewasisitiza wananchi wa Pugu mnadani kuilinda na kuitunza miundombinu ya reli ili kuiwezesha TRC kuendelea kutoa huduma ya usafirishaji kwa wananchi kupitia treni za abiria na treni za mizigo.
Pia amewakumbusha wananchi Ibara ya 27 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaelezea wajibu wa kila mwananchi kulinda mali na rasimali za Taifa, "Kila mwananchi anawajibu kwa mujibu wa ibara hii kulinda mali na rasilimali za Taifa ikiwemo miundombinu ya reli" amesisitiza ACP Mapala.
Vilevile ACP Mapala ameitaja Sheria namba 10 ya reli ya mwaka 2017 inakataza kuhatarisha usalama wa reli na watumiaji wa reli, uvamizi na kuingia bila ruhusa kwenye maeneo ya reli na wizi, Hivyo ametoa wito kwa wananchi kutofanya uharibifu wowote wa miundombinu ya reli.
"Napenda nitoe wito kuwa kila mwananchi analo jukumu la kuhakikisha miundombinu ya reli inalindwa na kuwa salama muda wote na yeyote atakayebainika kufanya uharibifu wowote kwenye uzio na mageti yaliyowekwa kuzunguka mradi wa SGR, Shirika la Reli Tanzania litamchukulia hatua kali za kisheria" alisema ACP Mapala.
Mwenyekiti wa mtaa wa Guluka kwalala Ndugu Augustino John Simba ameiomba TRC kuweka kivuko cha watembea kwa miguu mwisho wa lami kwaajili ya kurudisha mawasiliano ili kukidhi mahitaji ya kijamii ikiwemo masoko, shule na Zahanati kati ya Guluka kwalala na Mikongeni.
Katika hatua nyingine mwananchi wa Guluka kwalala Bwana Athumani Nguluko, ameishukuru TRC kwa kuendelea kutoa huduma ya usafiri wa treni ya mjini katika siku za kazi pamoja na siku ya jumamosi kati ya stesheni ya Dar es Salaam (Kamata) na Pugu Stesheni kwani huduma hii ya usafiri inarahisisha kufika kwa wakati katika shughuli za kiuchumi kila siku na kuwahi kurudi majumbani.
Zoezi la kampeni ya utoaji wa elimu shirikishi kwa wananchi kuhusu ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli ya SGR na MGR kwa awamu ya kwanza lilianzia Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoa wa Morogoro na kuendelea Mkoa wa Pwani ambako lilifanyika maeneo ya Magindu, Kwala na Soga na kumalizika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.