TRC YASHIRIKI KONGAMANO LA SIKU 100 ZA MHE. RAIS SAMIA

June
2021
Shirika la Reli Tanzania – TRC laadhimisha siku 100 za Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushiriki Kongamano la siku 100 za Mhe. Samia lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara - TNBC katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwl. Nyerere Juni 27, 2021.
Kongamano hilo limefanyika kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka Sekta binafsi, taasisi na mashirika ya umma kueleza na kujadili mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha siku 100 za Mhe. Samia Suluhu pamoja na kuona namna bora ya kuendeleza mazuri yaliyofanyika ndani za siku 100 za Mhe. Samia.
Mgeni Rasmi katika kongamano hilo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alifungua kongamano hilo amesema “Nawashukuru sekta binafsi kwa kuendelea kuunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Samia, naomba ushirikiano huu uendelee ili kwa pamoja tuweze kusonga mbele kwa kasi na kuendelea mbele” alieleza Mhe. Kassim
Akieleza baadhi ya mafanikio ya Mhe. Rais Samia Suluhu, Waziri Mkuu amesema kuwa Mhe. Rais ameendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaendelea kujengwa ikiwemo Reli ya Kisasa – SGR kutoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro hadi Makutupora Singida pamoja na kipande cha kutoka Isaka hadi Mwanza.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa alieleza majukumu ya Shirika ambayo ni usafirishaji wa mizigo na abiria pamoja na uendelezaji wa miundombinu ya reli kwa kukarabati na kujenga ambapo hivi sasa Shirika limejikita zaidi katika kujenga miundombinu mipya,
Kadogosa alisema kuwa “Katika kipindi cha siku 100 mradi wa SGR unaendelea vizuri ambapo kipande cha Dar es Salaam – Morogoro kimefika 92% na Morogoro – Makutupora Singida kimefika zaidi ya 62%, Mhe. Rais ameidhinisha Shilingi Bilioni 376.34 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli Mwanza – Isaka ambapo jiwe la msingi liliwekwa Juni 14, 2021 na ujenzi wake umeshaanza, pia Mhe. Rais ameelekeza kuanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Makutupora hadi Isaka”.
Kongamano la siku 100 za Rais Samia limefanyika baada ya Mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara lililofanyika katiia ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Mkuu ameeleza kuwa mkutano huo ulishindwa kuibua changamoto za sekta binafsi kwa kuwa changamoto nyingi zilizoibuliwa katika mkutano wa 11 mwa 2020 zilipatiwa ufumbuzi.