TRC YAJENGA UELEWA KWA WANANCHI KUELEKEA UWASHAJI UMEME SGR.
April
2022
Shirika la Reli Tanzania hivi karibuni limeendesha zoezi la utoaji elimu na uhamasishaji jamii kuhusiana na maandalizi ya upitishaji na uwashaji umeme katika miundombinu ya reli ya kisasa-SGR ,Aprili 22, 2022.
Zoezi hili la uhamasishaji na utoaji elimu kwa jamii limeanza katika kata ya Gongo la Mboto wilaya ya Ilala Jijini Dar Es Salaam likishirikisha wenyekiti wa serikali za mitaa ,wananchi mbali mbali katika kata hiyo pamoja na shule za msingi ikiwemo shule ya msingi Mikonge .
Aidha akiongea wakati wa zoezi hilo Mhandisi wa usalama na ulinzi wa Reli kutoka Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Fredrick Kitaly amesema kuwa zoezi la utoaji elimu na uhamasishaji kwa umma linalenga katika kuhakikisha jamii inapata elimu juu ya usalama wao hili kuhakikisha wanachukua tahadhari za kiusalama na kufuata miongozo itakayotelewa na wataalamu katika kipindi hiki ambacho zoezi la kupitisha umeme utakaotumika katika kuendesha treni ya kisasa unakwenda kuwashwa kwa mara ya kwanza katika miundo mbinu hiyo ya SGR.
"Zoezi hili la uhamasishaji na utoaji elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari za kiusalama limeanzia hapa Ilala lakini baadae zoezi hili litaendelea katika Maeneo mengine mbalimbali yanayopitiwa na Reli hii kwa kipande hiki cha kwanza kutoka Dar Es Salaam mpaka Morogoro ili wananchi hawa waweze kuchukua tahadhari za kiusalama katika kuhakikisha maisha ,afya na mali zao zinakuwa salama"Alisema Muhandisi Fredrick Kitaly
Miongoni mwa tahadhari zilizo ainishwa na Muhandisi Fredrick Kitaly ni kutogusa nyaya au uzio wa kituo cha umeme katika Reli,kuchukua tahadhari kabla ya kuvuka vivuko vya Reli,kuvuka vivuko vilivyoainishwa,kutofanya shughuli zozote za kijamii ,kiuchumi na kimaendeleo pembezoni mwa miundo mbinu ya Reli na mengineyo.
Nae mwenyekiti wa Mtaa wa Guruka kwa Lala kata ya Gongo la mboto Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam Bwana Augustine John amelipongeza Shirika la Reli Tanzania kwa kutoa elimu kwa wanachi kuhusu kuchukua tahadhari za kiusalama ambapo itasaidia katika kuepusha madhara na kujenga utamaduni wa wananchi kutunza miundo mbinu ya Reli .
"Zoezi hili limepokelewa vizuri sana na wananchi wangu wamelewa vizuri sana na nimatumaini watakuwa walimu wazuri kwa wengine"Alisema Bwana Augustine John.
Baada ya zoezi la upitishaji na uwashaji umeme katika miundo mbinu ya Reli ya Kisasa-SGR majaribio ya kwanza ya treni ya umeme kutoka kwa Mkandarasi anae jenga Reli hii kipande cha kwanza Dar es Salaam -Morogoro yanatarajiwa kuanza hivi karibuni Aprili 29,2022 .